Forum where rangeland experts, trainees and stakeholders meet to discuss and exchange social and scientific ideas for livestock production and range ecosystem sustainability.
Tuesday, 2 May 2017
Monday, 1 May 2017
Kwa ufupi kuhusu Sabi grass.
Kisayansi hujulikana kama Urochloa mosambicensis na kwa lugha za kawaida hujulikana kama Sabi grass (Australia), gonya grass (Zimbabwe) n.k.
Hizi ni nyasi zenye kustahimili ukame na kudumu zaidi ya mwaka mmoja (perennial). Hutofautiana kimo au wastani wa ukuaji pamoja na tabia (habit) ya ukuaji kutokana na sababu mbali mbali kama hali ya hewa ya eneo husika(climate), udongo (edaphic factors) n.k
Huota katika udongo tofauti ijapokuwa huitaji zaidi udongo wenye mbolea, kuanzia udongo wenye asili ya ufinyazi (clay soil) na ule wenye asili ya kichanga (sandy soil). Huweza kustahimili udongo wenye asili ya u-asidi, alkali na chumvi chumvi.
Hata hivyo, kwa nchini mwetu wafugaji wetu hawajajikita katika ulimaji wa nyasi aina hii lakini ni chanzo kizuri cha chakula kwa ajili ya mifugo.
Ni nyasi ambayo haijathibitika kuwa na sumu yoyote kwa mifugo au kuwa na uhusiano na magonjwa, hivyo ni chakula kisicho na madhara kwa mifugo.
Katika maeneo mengi hapa nchini aina hii ya nyasi hupatikana kwa kujiotea kwa asili. Mfugaji anaweza kuvuna na kuitunza nyasi hii kwa mfumo wa hei (hay) au saileji(silage).
Nyasi hizi hupendwa na mifugo zikiwa katika hali ya ubichi lakini pia zinapokuwa kavu(hay) bado mifugo huweza kula bila tatizo lolote.
Kwa mfugaji mwenye eneo lenye nyasi hizi anaweza kulitenga na kulitunza kwa ajili ya kuvuna nyasi na kuzitunza hadi msimu wa kiangazi. Labda tu, nyasi hizi hazina uwezo wa kustahimili mafuriko. Nyasi hizi hustahimili kuchungiwa lakini pia huweza kustahimili moto.
Imeandaliwa na makamu mwenyekiti-TRSA
Linus, Floidin John
Thursday, 27 April 2017
Kifo cha mzee wetu hakika ni pigo kwetu na wadau wa mifugo.
Sisi kama chama cha wanafunzi tunaosomea usimamizi na uendelezaji wa nyanda za malisho (TRSA), tunayo masikitiko makubwa sana juu ya kifo cha mzee wetu pia mwalimu wetu Mr. Protace.
Aidha taarifa hizi zimetushtua sana maana mara ya mwisho ni tulipomuona katika maonesho ya kumbukumbu ya waziri mkuu wa zamani wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, marehemu Mh. Edward Moringe Sokoine pale katika viwanja vya Chuo cha Kilimo cha Sokoine (Mazimbu campus).
Tunatoa pole kwa wanafamilia wote waliokutwa na msiba huu, idara ya sayansi ya wanyama, malisho na samaki (SUA), viongozi wa Chama cha Wadau wa Nyanda za malisho Tanzania (RST) na wadau wote walionufaika na ujuzi wa mzee wetu.
TRSA tunamuombea kwa mwenyezi Mungu amrehemu mzee wetu.
Tangulia mzee wetu hakika uliyoyafanya ni mengi sana na ni makubwa mno. Daima ulijaribu kutujenga katika misingi ya kupenda kila tulichokuwa tukikifanya. Ulitamani kila ulichokijua nasi tukifahamu kila ulipopata nafasi ya kuongea nasi. Yawezekana jitihada zako za kutupa ujuzi wako ilikuwa ni ishara ya ukomo wa maisha yako hapa duniani hivyo ulihitaji usiondoke na deni la kutompatia yeyote aliyetamani kuonja ujuzi wako wa kitaalamu.
Nyuma yako ni mbele yetu hakika
tunaomba mwenyezi Mungu akupumzishe salama.
Naamini siku moja tutakutana huko pia kwa
namna tofauti maana sote ni wapitaji hapa duniani.
Kile ulichotupatia nasi tutakitumia kuisaidia
jamii kama ishara ya kuenzi urithi uliotuachia
vichwani mwetu.
Tunawaombea wote waliopatwa na msiba huu, haswa familia yake pamoja na ndugu na jamaa Mungu awatie uvumilivu na moyo wa ujasiri katika kipindi hiki kigumu.
Familia ya wana-TRSA na wahitimu wa shahada ya usimamizi na uendelezaji wa nyanda za malisho tuko pamoja nanyi katika wakati huu mgumu.
Bwana alitoa na Bwana ametwaa
jina lake lihimidiwe.
Imeandaliwa na makamu mwenyekiti TRSA
Linus, Floidin John.
Saturday, 8 April 2017
Sekta ya mifugo itupiwe jicho la tatu...
Ukisoma sera yetu ya mifugo ya mwaka 2006 bonyeza hapa inaonesha jinsi gani kama taifa tuna ndoto ya kufikisha sekta ya ufugaji katika mfumo mpya na wakisasa zaidi. Inatoa maelekezo na namna ya kuendana na kasi ya ukuaji wa kiuchumi n.k. Lakini bahati mbaya tunatamani kufika katika
mafanikio tusiyoyawekea nguvu na nia thabiti ya kuhakikisha tunatekeleza matakwa ya sera yetu na kufikia katika
mafanikio tunayoyatamani.
Ni ukweli ulio wazi kuhusu
msululu mkubwa wa faida zinazotokana na ufugaji. Yawezekana ufugaji unashindwa
kuendelea sababu ya kufichwa nyuma ya pazia la kilimo. Pazia la kilimo kubeba
ufugaji limekuwa kikwazo kwa maendeleo ya mifugo kuanzia ngazi ya serikali hadi
kwa wananchi wa kawaida. Nasema hivi kwa sababu sekta ya kilimo na mifugo ni shughuli za kiuchumi ambazo kwa ujumla zinaenda pamoja. Na ndiyo maana hata Mheshimiwa Raisi John Pombe Magufuli akaamua kuziunganisha kuwa sekta moja. Lakini ufugaji umekuwa ukitembea chini ya kivuli cha kilimo. Tunashuhudia fursa nyingi zikirudi upande wa kilimo mfano, utoaji wa ruzuku, mikopo, mbegu za mazao (kilimo) hakuna mbegu za malisho, ardhi, masoko bora, mbolea, kilimo cha umwagiliaji n.k . Huduma sawa na zinazopelekwa kwenye kilimo tulitegemea pia zielekezwe kwenye kuinua ufugaji lakini ni tofauti kabisa. Mchango wa ufugaji ijapokuwa ni mkubwa katika uchangiaji wa mapato ya halmashauri mbalimbali, mfano minada lakini umekuwa hauleti mrejesho sawa na
nguvu ya kuhakikisha uboreshwaji wa ufugaji unazingatiwa.
Sekta ya mifugo inakua kwa kasi
ya kusuasua sababu ya ukosefu wa mipango madhubuti. Ukuaji wake unategemea
zaidi ukuaji wa kipato kwa mfugaji na
taifa kwa ujumla ikisaidiwa na ukuaji wa
teknolojia na miundombinu.
Matatizo ya ukosefu wa teknolojia
thabiti kama mbegu bora za ng'ombe wa maziwa na nyama yamesababisha kudunisha
sekta hii ya mifugo hapa nchini. Lakini hatuwezi kupuuzia mchango wa mapungufu
ya kisera na kisheria hapa nchini katika kuchangia kudolola kwa sekta ya
mifugo.
Bahati mbaya zaidi serikali
imeshindwa kuweka mazingira salama ya kuhakikisha ufugaji unanufaika na
ongezeko la watu hapa nchini. Tunategemea ongezeko la watu liendane na uhitaji
mkubwa zaidi wa mifugo na mazao yake hivyo lazima uzalishaji uongezeke zaidi,
lakini je ni kweli hapa nchini Iko hivyo?
Tunashudia uharibifu mkubwa wa
maeneo ya malisho sababu ya ongezeko la watu na kuvamia maeneo ya malisho
kiholela, kilimo cha kuhama hama n.k. Wafugaji wanafuga kiholela na kimazoea sababu ya ukosefu wa elimu ya kutosha.
Wafugaji wetu ni wafugaji wenye ufugaji wa kurithishana. Hivyo hata namna ya ushughulikiaji wa mifugo lazima uendane na namna alivyokua akiona wakubwa wake wakihudumia mifugo. Hatutegemei wafugaji kubadilika bila kuweka nguvu na jitihada za dhati kuwabadilisha.
Yawezekana hata wataalamu wenyewe wakakata tamaa sababu ya wafugaji kutobadilika. Lakini haina budi kuzidi kuwasaidia maana ufugaji kwao ni utamaduni. Kupambana na utamaduni kuwarudisha kwenye mtizamo wa kiuchumi lazima kupambana nao taratibu.
Mahitaji ya wafugaji serikali iyaangalie upya kama mikopo, ruzuku kwenye madawa, mbegu za malisho n.k ili kuchochea ukuaji wa sekta ya mifugo. Sekta ya mifugo isitembee chini ya kivuli cha kilimo.
Niiombe serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, wadau na jamii kwa ujumla kushirikiana kumkwamua mfugaji. Lakini na wafugaji wetu wawe tayari kupokea mabadiliko haya.
IMEANDALIWA NA MAKAMU MWENYEKITI TRSA
Linus Floidin John.
Thursday, 30 March 2017
KUSTAWISHA SHAMBA LA NYASI KATIKA NYANDA KAME.
Chanzo; CHAMA CHA NYANDA ZA MALISHO TANZANIA (RST).
P.O.BOX 3004, CHUO KIKUU MOROGORO- TANZANIA.
Changamoto za kustawisha shamba la nyasi.
| Mifugo katika machunga ya jumuiya |
ü
Machunga mengi nchini ni ya jumuiya nani
astawishe nyasi?
ü
Mifugo inaranda randa hovyo kwa hiyo ni vigumu
kustawisha mashamba binafsi ya malisho
ü
Uhaba wa mbegu za malisho na utaalamu wa
kustawisha malisho vijijini unadhoofisha ari ya kupanda malisho.
Kuongeza wingi wa mbegu za nyasi.
ü
Ili kuongeza wingi wa mbegu za nyasi panda kitalu cha nyasi kwa
kutumia vishina vya nyasi.
ü
Chimba kijaluba chenye kina cha sentimeta 40 na
upana wa sentimeta 100 na urefu wa sentimeta 500.
ü
Weka ndoo 5 za samadi na mbolea ya kupandia
(DAP) gramu 500.
ü
Halafu panda vishina vya nyasi sentimeta 25 X
25.
Kustawisha shamba la nyasi.
| Kitalu cha nyasi kilichopandwa |
ü
Chimba mitaro yenye kina cha sentimeta 40 kwa
trekta au jembe la kukokotwa na ng’ombe; nafasi kati ya mitaro ni sentimeta 50.
ü
Changanya mbolea zote na udongo vizuri.
ü
Mvua inaponyesha na kukolea vizuri panda vishina
vya nyasi toka katika kitalu cha nyasi.
ü
Palilia shamba la nyasi wiki la tatu na la sita
baada ya kupanda.
ü
Weka mbolea ya kukuzia kilo 50 kwa ekari moja
katika wiki la tatu baada ya kupanda.
Kuvuna shamba la nyasi.
ü
Vuna nyasi siku 84 baada ya kupanda kabla ya
hapo mizizi inakuwa haijakua vizuri.
ü
Vuna nyasi kiasi cha sentimeta 15 juu ya ardhi. Vuna kila nyasi zinapotoa maua.
ü
Sambaza samadi, DAP kilo 50 na mbolea ya kukuzia
kilo 50 kwa ekari kila mwaka mvua zinapoanza.
| Shamba la nyasi lililostawi vizuri. IMEANDALIWA NA MAKAMU MWENYEKITI TRSA LINUS FLOIDIN JOHN. |
Wednesday, 22 March 2017
MATUMIZI YA MABUA(STRAWS) KWA AJILI YA MIFUGO
Monday, 20 March 2017
UMUHIMU WA MTI WA MLUSINA KATIKA UFUGAJI.
![]() |
| Leucaena leucocephala |
Kwa kiingereza huitwa Leucaena au Lead tree.
Kiswahili huitwa mti wa Mlusina.
Mmea huu jamii ya mikunde(leguminous) asili yake ni Mexico. Lakini hapa nchini pia hustawi vizuri kabisa. Ni kati ya miti yenye jamii ya mikunde inayokua kwa haraka
sana. Ni chanzo cha chakula kwa mifugo . Hupandwa pembeni ya shamba kama
kuonesha mpaka wa shamba, kutoa kivuli, kizuia upepo(wind breaker), kuzuia mmomonyoko wa
ardhi au maalumu kwa ajili ya chakula cha mifugo. Mti huu ukiachwa kwa takriban
mwaka 1.5 huruhusu mzizi mkuu kuingia ndani zaidi ya udongo hivyo kuhakikisha uzalishaji wa chakulacha
mifugo hata wakati wa kiangazi kipindi ambacho hakuna chakula cha kutosha au ubora
wa malisho unapokuwa mbovu.
Shina laini na majani
yake ni chanzo kizuri cha protini kwa mifugo na virutubisho vingine kama carotenoids na vitamins, lakini pia huambatana
na asidi-amino iitwayo mimosine ambayo huwa na athari endapo chakula kinachotokana na
jamii hii ya mikunde kitatumiwa pasipo uangalifu, haswa wanyama wenye tumbo
moja(monogastric) kama nguruwe, kuku na sungura huathirika zaidi na huweza kusababisha kifo kwa wanyama hawa.
Mlusina hufananishwa na mkunde mwingine (alfaalfa) muhimu kwa wingi wa virutubisho haswa protini kwa ajili ya mifugo. Lakini Mlusina una upungufu wa sodium na iodine lakini una wingi wa b
-carotene.
MAANDALIZI YA MLUSINA KWA AJILI YA MIFUGO
![]() |
| Majani ya mlusina yaliyoandaliwa kama chakula cha mifugo |
Maandalizi ya mlusina kwa ajili ya chakula cha mifugo huandaliwa kwa kuondoa majani pekee kutoka kwenye matawi ya mlusina. Ni kwa sababu ndiyo sehemu ya mmea huu yenye kuwa rahisi zaidi kutumiwa na mifugo(digestible and palatable). Shina (stem) nalo huweza kutumika lakini labda sehemu changa kabisa kwa sababu ya changamoto ya tannins.
Majani haya hukaushwa juani ili kudhibiti madhara yatokanayo na asidi-amino ya mimosine ambayo ina athari kwa mifugo. Baada ya majani kupoteza kiasi cha maji ilichobeba, huwa tayari kwa ajili ya kuendelea na taratibu zingine za kuandaa chakula cha mifugo.
| Majani ya Mlusina yaliyokaushwa |
Chakula kilichoadaliwa kwa ajili ya kuku huwekewa 5%
ya majani ya mlusina, chakula kwa ajili ya nguruwe kinatakiwa kuwa na 10% tu
ya mchanganyiko wa majani ya mlusina na chakula kinachoandaliwa kwa ajili ya
ng’ombe kinatakiwa kisichukue zaidi ya
30% ya mchanganyiko wa majani ya mlusina (Dongjing na Guodao, 1994).
Mlusina ni mzuri kwa sababu unapunguza gharama za kununua chakula cha kurutubishia mifugo(concentrates).
Hata hivyo, makala hii inajikita kwa matumizi ya Mlusina kwa ng'ombe. Maandalizi ya chakula kwa ajili ya ng'ombe yanatakiwa yasizidi 30%. Mfano kama chakula kinachoandaliwa ni kilo 100 maana yake ni kwamba majani ya Mlusina ambayo ni chanzo cha protini yanatakiwa yasizidi kilo 30. Hata hivyo athari nyingi huonekana endapo asilimia za Mlusina zitazidishwa kwa kipindi kirefu, athari hizo ni kama vile kunyonyoka nywele(alopecia), matatizo katika ulaji(anorexia), kupoteza uzito, kutokwa na ute mdomoni(deep salivation), kuchubuka utumbo(esophagus lesions), kupoteza seli kwenye rumen na reticulum (necrotic papillae in the
rumen and reticulum), kuvimba kwa tezi (thyroid hyperplasia), kiasi kidogo cha homoni ya thyroxine(T4) kwenye damu, kifo cha kiinitete na vifo vya kabla na baada ya kuzaliwa (early embryonic mortality and perinatal death) (Allison et al., 1992; Al-dehneh et al., 1994).
Ni vema mfugaji akawa na huu mmea ndani ya shamba lake kwa ajili ya mifugo yake kupata protini kwa wingi bila kutumia fedha nyingi kugharamia vyakula vya protini vinavyouzwa kwenye maduka mbalimbali ya vyakula vya mifugo.
IMEANDALIWA NA MAKAMU MWENYEKITI TRSA
Linus Floidin John.
Sunday, 19 March 2017
UVUNAJI WA MAJI MAENEO YENYE CHANGAMOTO YA UKAME NI UKOMBOZI WA UFUGAJI.
![]() |
| Mfumo wa kuvunia maji yanayotiririka. |
Uvunaji wa maji (rain water harvesting) ni teknolojia inayotumika kukusanyia na kutunzia maji kwa ajili ya shughuli mbalimbali. Hata hivyo kuna njia nyingi au aina tofauti za uvunaji wa maji.
Hata hivyo makala ya leo ni kutoa mtizamo wangu kwa wafugaji wa kitanzania(pastoralists) wanaoishi ama kufanya shughuli za ufugaji katika mikoa yenye changamoto ya ukame, mfano Dodoma, Manyara, Singida, Shinyanga na baadhi ya maeneo ya Morogoro.
Wafugaji wa kitanzania wamekuwa wakiathiriwa sana na tatizo la uchelewaji wa mvua za vuli. Husababisha ukosefu wa malisho na maji kwa ajili ya mifugo na wafugaji wenyewe. Aidha, kutotabirika kwa mvua pamoja na kiwango kidogo cha mvua ni changamoto katika shughuli ya ufugaji hapa nchini.
Katika msimu wa ukame wafugaji wamekuwa wakihama kutoka sehemu moja hadi nyingine kuhakikisha kwamba wanapata mahitaji ya mifugo yao kama vile malisho na maji. Hata kama sehemu wanazoishi zina nyasi bado hulazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta maji kwa ajili ya mifugo. Kuhama hama kumekuwa kukisababisha hasara nyingi sana kama vile, migogoro ya mara kwa mara, uharibifu wa vyanzo vya maji, kupoteza muda mwingi ambao nguvu kazi ingetumika kufanya shughuli nyingine za kimaendeleo, kukosesha haki watoto ambao wana umri wa kwenda shule, uzalishaji hafifu wa mifugo sababu mifugo hutumia nishati kubwa sana kusafiri umbali mrefu hivo kupunguza ufanisi wa kushika mimba, ukuaji na uzalishaji wa maziwa na nyama iliyo bora zaidi.
Hata, hivyo wafugaji wetu wanaweza kutumia teknolojia mbadala ya kuvuna maji wakati wa masika na kuyatunza hadi msimu wa ukame kipindi ambacho kuna changamoto ya maji. Kiasi kikubwa cha maji wakati wa msimu wa mvua hutiririka juu ya uso wa dunia (surface run-off) na kusababisha matatizo makubwa kama mafuriko, mmonyoko wa ardhi na uharibifu wa miundombinu.
![]() |
| Eneo lililoathirika na mafuriko |
Matatizo haya yamekuwa yakitokana na uwanda mkubwa unaokuwa tambarare na wenye ukosefu wa uoto wa kutosha kuzuia madhara ya maji yanayotiririka kwa kasi. Hata hivyo hatuwezi kupuuzia changamoto ya ubovu wa miundo mbinu katika kuchangia tatizo la mafuriko haya.
Wafugaji wana uwezo mkubwa sana wa kutumia fursa ya mvua inayonyesha ndani ya muda mfupi kwa mwaka katika maeneo yao kwa ajili ya kupambana na chanagamoto zinazosababishwa na ukame kwa upande wa ufugaji. Ni dhahiri kabisa, suala la mabadiliko ya tabia ya nchi linaathiri kila sekta hapa nchini. Hivyo basi, hata serikali tunayoitegemea ina kazi kubwa kupambana na mabadiliko haya kwa sekta zote. Lakini suala la uvunaji wa maji bado wafugaji wanaweza kulifanya kwa ufanisi mkubwa pasipo kuhitaji msaada wa kifedha kutoka serikalini labda tu ushauri wa kitaalamu pekee. Wafugaji wana hazina kubwa, mifugo ni hazina iliyobeba utajiri wa wafugaji. Wanatakiwa kujifunza kutokana na hasara kubwa wanayopata kila mara tunapokumbana na hali ya ukame hapa nchini. Kuna njia rahisi za kuvuna maji bila kutumia vifaa na zana za gharama kubwa kuandaa eneo la kuvunia maji. Kwa hazina ya mifugo waliyonayo wafugaji si jambo kubwa wala gumu kutumia hata teknolojia za asili (local technology) kuandaa eneo la kuvunia maji yatirirkayo msimu wa mvua.
![]() |
| Teknolojia ya asili ya kuvunia maji |
Huweza kufanywa kwa kufata mkodo au mteremko wa uelekeo wa maji lakini pia kama eneo linabeba kiasi kikubwa cha maji njia ya kuhamisha(divert) baadhi ya kiasi cha maji kuelekea eneo la kuvunia huweza kutumika pia.
![]() |
| Teknolojia ya asili ya kuvunia maji |
FAIDA ZA KUVUNA MAJI.
Faida za kuvuna maji ni nyingi sana,lakini ntajaribu kuorodhesha baadhi tu,
- Kunyweshea mifugo msimu ambao maji hayapatikani ndani ya eneo husika kutoka kwenye vyanzo vingine.
- Matumizi ya nyumbani kwa ajili ya familia.
- Kumwagilizia malisho kama mfugaji ataamua kuzalisha malisho kwa ajili ya mifugo yake, hivyo kuhakikisha uwepo wa chakula cha mifugo.
- Kupunguza tatizo la mmomonyoko wa ardhi.
- Kupunguza tatizo la mafuriko kama kiasi kikubwa cha maji kitavunwa ili maji yasipotee bure.
- Kuboresha hali ya ufugaji, sababu mifugo haitosafiri umbali mrefu kutafuta maji hivyo nguvu kubwa ya mnyama itaelekezwa kwenye ukuaji na uzalishaji.
- Kupunguza tatizo la migogoro na watumiaji wengine wa ardhi.
IMEANDALIWA NA MAKAMU MWENYEKITI TRSA
Linus Floidin John.
Saturday, 18 March 2017
KILIMO CHA MALISHO NI MUHIMU SANA KWA UFUGAJI WENYE TIJA
| Gwatamala |
Kwa kiingereza huitwa Guatemala grass.
Na kiswahili chake hujulikana kama nyasi aina ya Gwatemala.
Asili yake ni kutoka nchini Mexico. Ni nyasi ambazo hudumu kwa muda mrefu(perennial), Huota na kukua kwa kusimama(erect) kwa urefu wa mita 2-3.
Huchomoza matawi kutoka kwenye vinundu(nodes) vya juu.
Hupandwa kwa kutumia vishina katika kipindi cha mwanzo wa msimu wa mvua.
| Mfano wa vishina , kushoto ndiyo mfano wa kishina kilichoandaliwa kupandwa. |
Hupandwa ndani ya mashimo ambayo yanakuwa umbali wa sentimita 50-65 kati ya shimo na shimo ili kutoa nafasi ya kutosha baina ya nyasi. Hupandwa katika mistari na kati ya mstari mmoja na mwingine iwe ni mita 100.
Mfano wa jinsi ya kupanda vishina vya gwatamala.
|
Mfugaji anaweza kuandaa shamba na kupanda nyasi za gwatamala kwa ajili ya mifugo. Mahitaji ya kilimo hiki ni kwenye udongo wenye rutuba, Gwatamala huitaji 400 kg nitrogen, 80 kg phosphorus, 50 kg
potassium, 50 kg calcium na 50 kg za magnesium kwa mwaka kwa hekta (Risopoulos, 1966).
Ijapokuwa nyasi hizi hupendelea sehemu zenye mvua ya kutosha lakini pia huweza kukua vizuri katika maeneo yenye udongo mzuri yanayopokea mvua kwa wastani wa 600mm kwa mwaka. Na wakati wa kiangazi hupunguza uwezo wa kuzalisha malisho. Hustahimili ardhi yenye asidi na aluminium lakini nyasi hizi hazistahimili maeneo yenye tatizo la kukumbwa na mafuriko.
Nyasi huweza kuwa tayari kuvunwa miezi sita baada ya kupandwa lakini huchukua tofauti ya miezi minne tu kuvunwa msimu kwa msimu.
Ni nyasi nzuri kwa ajili ya ng'ombe wa maziwa kwa kukata na kulisha (green chop-chop for
zero grazing) lakini pia nyasi za gwatamala zinaweza kutunzwa kwa mfumo sileji kwa ajili ya matumizi ya baadae katika msimu wa kiangazi.
IMEANDALIWA NA MAKAMU MWENYEKITI TRSA
Linus Floidin John.
Friday, 17 March 2017
UKIJALI ARDHI (MACHUNGA) UTAJALI MIFUGO PIA
![]() |
| MIFUGO IKIWA MACHUNGANI |
Stocking rate
ni idadi ya mifugo inayoweza kuchungwa ndani ya eneo fulani kwa muda maalumu.
Hii ni muhimu
sana kwa sababu inahakikisha hali salama ya ardhi na ufanisi(uzalishaji) wa
mifugo hivo ni chanzo cha faida(kipato) ya ufugaji pamoja na kuyapa malisho
uwezo wa kurudi katika hali yake ya awali(resilience). Idadi ndogo ya mifugo
kwenye machunga ni nzuri si tu kwamba
inadumisha hali ya usalama wa udongo lakini pia ni njia sa kurekebisha eneo
lililoathiriwa(poor land condition).
Kwa
kawaida hali ya udongo huwa mbaya kiuzalishaji endapo malisho yatatumika (utilization)
kwa zaidi ya 30%. Hapa namaanisha uzito (weight) wa jani(grass) ni 100% hivyo
basi ikipotea kuanzia 70% ndiyo hatari inayomaanishwa.
Idadi ya mifugo(stocking rate) inatakiwa isizidi au
kuwa sawa na uwezo wa ardhi (carrying capacity) kuhudumia mifugo. Hii itasaidia
mimea kuendelea kuzalisha(photosynthesis), kuimarisha hali ya udong(soil
stability), ulinzi wa mfumo wa maji(watersheds) na kukidhi mahitaji ya viumbe
vingine kama wadudu(insects) na wanyama pori(wild animals).
Mahitaji makubwa ya mifugo ni maji na malisho,
mahitaji haya hubadilika sana ndani ya mwaka kutokana na sababu mbalimbali kama
vile ukame n.k. Hata hivyo mahitaji ya mfugaji ni kuhakikisha kuwa shughuli
yake ya ufugaji inatanuka zaidi ili kumpatia kipato zaidi. Hivyo kutokana na
sababu nyingi zilizo nje ya uwezo wa mfugaji kama vile ugumu wa upatikanaji wa
mbegu bora zenye kuzalisha kiwango kikubwa cha nyama au maziwa,
![]() |
| NG'OMBE WA NYAMA AINA YA BONSMARA |
mfugaji
hulazimika kutumia mbegu za asili(ng’ombe) zenye vinasaba hafifu katika
uzalishaji na ukuaji, lakini hapa huitajika kuwa na idadi kubwa zaidi ili
kukidhi mahitaji.
| NG'OMBE WA ASILI |
Kutokana na hizi changamoto za machunga ya jumuiya
ni changamoto kusimamia idadi ya mifugo katika eneo husika haswa kwa kuzingatia
ufugaji wa kuhamahama, machunga hupitia misimu ya kuelemewa na mifugo na misimu
ya kupungua mifugo kutokana na uwepo wa malisho na /maji.
Lakini ni muhimu kuelewa uwezo wa ardhi kuzalisha
malisho. Hii inaweza kutathiminiwa kwa kutumia kiwango cha malisho(standing
crop end of growing season) mwanzo wa msimu wa kiangazi.
Tabia hatarishi ndani ya machunga zinazotokana na
idadi kubwa lazima zifatiliwe ili kuzigundua mapema na kudhibiti idadi ya
mifugo. Idadi ya mifugo ndani ya machunga lazima idhibitiwe ili kulinda
ikolojia na ardhi iweze kuhudumia mifugo kwa ufanisi mkubwa.
IDADI YA MIFUGO INAWEZA KUKADIRIWA KWA HATUA KUU
NNE.
4-step Procedure outlined by Holechek (1988)
- Calculate total usable forage
- Adjust total usable forage
- Calculate forage demand
- Balance supply/demand to stocking rate
Only useful to get a “guess” of initial
stocking rat
Hatua hizi zitajadiliwa wakati mwingine…..
IMEANDALIWA NA MAKAMU MWENYEKITI TRSA.
KUUZA MIFUGO ISIONEKANE KAMA TU NDIYO NJIA PEKEE YA KUKABIRI MSONGAMANO WA MIFUGO KWENYE MAENEO YA MACHUNGA.
![]() |
| ARDHI ILIYOATHIRIWA NA SHUGHULI ZA UFUGAJI |
Hapa lazima tuoneshe utofauti wa mtaalamu wa usimamizi na
uendelezaji wa nyanda za malisho na wataalamu wengine.
Ni kweli ndani ya nchi yetu tunakabiriwa na maeneo yenye
kuathiriwa na mikusanyiko ya mifugo eneo moja na kusababisha uharibifu wa
mazingira na migogoro. Mikusanyiko hii chanzo chake ni katika hatua za
utafutaji wa malisho, maji, kukimbia magonjwa ya mifugo na sababu zingine za
kijamii.
Mikusanyiko hii imeathiri ardhi na kusababisha mmomonyoko wa ardhi na
makorongo, uharibifu wa vyanzo vya maji, migogoro ya mara kwa mara na uharibifu
wa malisho.
Hata hivyo mikusanyiko hii imeonekana kuzidi kuongezeka
kadri siku zinavyokwenda maana yake ni kwamba wafugaji wetu wanakumbana na
changamoto nyingi machungani.
Ukisikiliza majadiliano ya watu wengi wanasema kuwa wafugaji
wanatakiwa kutambua kuwa sasa ardhi imekuwa na matumizi mengi lazima wajifunze
kutulia sehemu moja na kuzalisha kitaalamu na kisasa zaidi. Ni kweli lakini
mabadiliko haya yanapofanyika wahusika wakuu hawaangalii mbadala wa wafugaji
waliokuwa wanatumia maeneo haya, hatimaye hutoa nafasi ya wafugaji
kutangatanga.
Mfugaji anakabiliwa na marekebisho ya matumizi ya ardhi
yasiyojali mazingira rafiki ya shughuli yake.
Ufugaji unaonekana kama shughuli inayostahili kufanyiwa
kwenye maeneo yasiyofaa kwa kilimo(remote & unproductive areas), lakini
binafsi hii hoja huwa naipinga kwa sababu kuu mbili,
1)Tukisema ufugaji ufanyike katika maeneo yasiyofaa kwa
kilimo, swali ni Je,katika karne hii yenye teknolojia za juu sana ni eneo gani
lisilofaa kwa kilimo?. Mfano, teknolojia za umwagiliaji,mbegu bora za nafaka na
mbolea.
2) Mahitaji ya malisho ni sawa kabisa na mazao ya nafaka,
mfano mbolea ya kutosha na maji, vyote hivi hutimiza mahitaji ya mwili wa
mnyama ili kufikia uzalishaji wenye tija zaidi na bora kwa mtumiaji.
Kwa kiwango kikubwa misongamano au mikusanyiko hii
inasababishwa na watumiaji wengine wa ardhi wasiotoa mbadala wa mfugaji kupata
mahitaji yake.
Mfano,
ü
Kumzuia mfugaji kuharibu vyanzo vya maji ni
vizuri sana, lakini kumzuia mfugaji pasipo kumtengenezea njia mbadala ya
kunyweshea mifugo yake pasipo kuathiri vyanzo vya maji ni mbaya zaidi.
ü
Kumwondosha mfugaji katika ardhi yenye rutuba
ili kupanua shughuli za kilimo ni vema lakini kumwondosha bila kumwandalia
sehemu nyingine yenye mahitaji stahiki ni kumwonea.
ü
Kumwondoa mfugaji ili apishe uwekezaji ni vema
kwa uchumi wa nchi, lakini hatari ni pale asipoandaliwa eneo zuri la
kuhamishiwa.
ü
Upanuzi wa maeneo tengefu(reserves) kwa ajili ya
mapori na wanyama pori ni vizuri lakini unapomuondosha eneo husika
unamtengenezea mbadala gani?
ü
Kukabidhi mamlaka ya vijiji kutenga maeneo ya
malisho, ni vizuri lakini watu hawa wana elimu ya mifugo na wanajua ni maeneo
gani na yenye sifa gani yanafaa kwa ajili ya mifugo?
Hiyo yote ni baadhi ya mifano
inayosababisha mikusanyiko mikubwa ya mifugo kutokana na kukimbia sehemu
mbalimbali zenye changamoto. Hivo ni ukweli kwamba kwa asilimia kubwa
misongamano hii inasababishwa na watumiaji wengine wa ardhi japo mfugaji ndiye
anaonekana tatizo.
KUPUNGUZA WINGI WA MIFUGO ENEO MOJA BILA KUUZA MIFUGO.
Hapa ndipo mtaalamu wa malisho
anaweza kutofautiana na maamuzi ya wataalamu wasio wa machunga wasiojua sifa za
mifugo kwenye machunga(grazing behavior).
Ø
Miundombinu ya maji, hii inaweza kuwa suluhisho
la misongamano na kupunguza mikusanyiko ya mifugo kwenye machunga pasipo kuuza
mifugo. Kupangilia umbali wa vituo vya maji(water sources) kulingana na aina ya
mifugo iliyopo ndani ya machunga.Hii itasaidia kupunguza msongamano.
Ø
Kubadilisha maeneo ya kuchungia kufatana na
umri, breed na spishi(species). Mfano, ndama wanaweza kuchungiwa maeneo yenye makorongo,
mteremko mkali (rough terrain) hii pia itapunguza msongamano.
Ø
Kuwa na spishi tofauti ya mifugo hii itasaidia
mifugo ya spishi tofauti kuweza kutumia aina tofauti ya aina ya mimea na maeneo
tofauti.
Ø
Kagua eneo la machunga yawezekana msongamano wa
malisho unasababishwa na uvamizi wa vichaka, mimea vamizi, magonjwa au wadudu
hatarishi kama ndorobo n.k.
Utaalamu wowote ndani ya machunga ni vyema ukatizama
kuongezea ardhi uwezo wa kuhudumia mifugo mingi zaidi ili kustawisha ufugaji
hapa nchini.
IMEANDALIWA NA MAKAMU M/KITI TRSA
Tuesday, 14 March 2017
TUJADILI KIDOGO KUHUSU NDOROBO (TSETSE FLY) TANZANIA.
Ndorobo ni wadudu warukao ambao husambaza trypanosomes wasababishao magonjwa ya trypanosomiasis na nagana kwa mifugo na malale kwa binadamu. Kwa Tanzania trypanosomiasis ni kati ya magonjwa yanayoathiri binadamu na mifugo. Ndorobo wana madhara mengi sana kwa mifugo kama vile kuongezeka kwa vifo, mimba kutoka, kushuka kwa uwezo wa kuzaliana, ukuaji hafifu, uzalishaji hafifu wa nyama na maziwa, kuzuia matumizi ya machunga,kuongeza gharama za kuzuia ndorobo n.k. Kwa Afrika inakadiriwa kuwa ni kilomita za mraba milioni 10 zenye ndorobo ambapo kati ya hizo ni takribani kilomita za mraba milioni 7 zinazostahili kwa kulishia mifugo na eneo lililobaki likiwa ni misitu.
Ni 40% ya eneo la Tazania lililoathiriwa na ndorobo ambalolingefaa kwa shughuli za kilimo na kuchungia mifugo. Aidha anasema ni takribani mifugo milioni 4.4 na watu milioni4 ambao wako kwenye nafasi kubwa ya kuambukizwa ugonjwa unaotokana na ndorobo. Inakadiriwa kuwa ni takribani US$ 7.98 milioni zinapotea kila mwaka kutokana na madhara yatokanayo na ndorobo (Malele,2011). Kwa kiasi hiki cha pesa inatoa nafasi kubwa kutafakari ni kwa jinsi gani taifa na wafugaji wanapoteza mapato kama tu ndorobo wangedhibitiwa.
Tanzania inakadiriwa kuwa na spishi(species) kumi (10) za ndorobo ambazo zimetapakaa kulingana na uwezo wa kila spishi kustahimili eneo husika. Aidha inaelezwa kuwa, kubadilika kwa matumizi ya ardhi, ongezekola watu na shughulu zinazohusu binadamu ni kati ya vyanzo vya kusambaa kwa ndorobo hapa nchini.
NJIA ZA KUDHIBITI NDOROBO
. 1. Kuondoa vichaka. Hii ni njia iliyoanza kutumika tangu enzi za ukoloni. Ilihusisha kuondoa aidha vichaka vyote au sehemu tu ya vichaka iliyoonesha kuwa kivutio ama makazi ya ndorobo. Kwa upande wa mazingira si rafiki sababu husababisha eneo kuwa wazi hivo kuwa na madhara mengi. Hivo haitumiki sana ijapokuwa inaweza kutumika kwa kuzingatia usalama wa mazingira. 2.2. Kutumia kemikali
Hii ni njia ya kutumia dawa ya kuulia wadudu ambapo inaweza kupuliziwa kutoka angani(aerial spraying) kwa kutumia vifaa maalumu ama kupuliziwa kutokea ardhini(ground spraying), kila njia ina madhara yake na faida zake na viumbe vingine pia huweza kuathirika kutokana na kemikali inayotumika kuua ndorobo.Kemikali zinazoweza kutumika ni Dieldrin (a residual organochloride), Endosulfan (Thiodan; a non-residual organochloride) na Synthetic pyrethroids.3. Sterile male release technique
Hii ni njia inayotumika kwa kuandaa madume ya ndorobo ndani ya maabara.Madume haya huondolewa uwezo wa mbegu zake kutungisha halafu huachiliwa kwenye eneo liliothiriwa na ndorobo. Ni njia ya gharama sana. Ijapokuwa kutokana na (Bonomi et al., 2011),G. fuscipes ina onekana kuwa tofauti katika njia hii. Njia hufanya ufanisi zaidi kama eneo linalokusudiwa ni dogo pia idadi ya madume yaliyo ondolewa uwezo wa kutungisha maabara yanatakiwa kuwa na idadi kubwa kuliko madume yaliyoko eneo husika.4. Kutumia mitego
Hutengenezwa kwa kutumia kitambaa cheusi na bluu. Rangi nyeusi huwavuta ndorobo na kutua kwenye rangi nyeusi hivyo kuweza kuvutwa kwenye kifaa cha kukusanyia au sehemu ilikopakwa kemikali ya kuua ndorobo. Lakini pia kemikali za kuwavutia kama acetone, mkojo wa ngombe au mbogo huweza kutumika sababu hutoa harufu ya kuwavuta. Kuzingatia, kuna mitego ya aina nyingi kulingana na aina(spishi) ya ndorobo.Hizo ni baadhi ya njia za kudhibiti ndorobo ambazo hutumika katika maeneo yaliyo athirika na ndorobo.
IMEANDALIWA NA MAKAMU M/KITI TRSA
Tuesday, 7 March 2017
TUJIFUNZE KULINGANA NA MAKOSA.
Huu ulikuwa ni mwaka ulioacha simanzi kubwa baina ya wafugaji ama jamii zinazotegemea shughuli ya ufugaji kwa ajili ya kuendeshea maisha yao. Simanzi hii imesababishwa na kuchelewa kwa mvua kulikosababisha kukosekana kwa malisho na maji kwa kiasi kikubwa hapa nchini na takribani ukanda wetu wote wa Afrika mashariki.
Ni ukweli usiopingika kwamba madhara yatokanayo na uchelewaji wa mvua za vuli si mara ya kwanza kuyashuhudia hapa nchini. Kumekuwa na upotevu wa idadi kubwa ya mifugo inayokufa sababu ya ukosefu wa malisho na maji ndani ya msimu wa kiangazi. Lakini swali ni moja kwamba NI KWELI TUNAJIFUNZA KUTOKANA NA MAKOSA?.
Hapa hakuna wa kulaumiwa kuhusu mabadiliko ya tabia ya nchi lakini alaumiwe yule mwenye uwezo wa kufikisha elimu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi. Katika nchi yetu kuanzia wasomi na hata wale wasio na elimu ya darasani swala la kilimo cha malisho ni wimbo usioeleweka masikioni mwao. Lakini je, tuache kuchukua njia sahihi kwa sababu ya ukosefu wa uelewa juu ya swala hili?
Kilimo cha malisho ndio njia pekee ya kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi. Ni njia itakayomwezesha na kumuhakikishia mfugaji uhakika wa chakula cha mifugo wakati wa kiangazi. Mfugaji mwenye kuweza kudhubutu kulima malisho atakuwa na uwezo wa kuvuna na kuweka akiba ya malisho(kipindi cha msimu wa masika) na kutumia akiba hiyo kipindi cha kiangazi wakati ambapo kuna upungufu mkubwa wa malisho. Jukumu hili linabaki kwenye mamlaka husika kuhakikisha mbegu za malisho bora zinapatikana ili elimu ya kilimo malisho iambatane na mbegu za malisho.
Katika kipindi hiki ambacho mifugo mingi inakufa tusiwalaumu wafugaji kwa kuwaambia hawataki kuuza mifugo haswa msimu wa kiangazi wakati tunajua mapungufu ya soko letu la mifugo na mazao yake. Tusiwalaumu kutangatanga wakati tunajua hali ya machunga hapa nchini. Tunao uwezo wa kukomboa ufugaji na ukaendelea kushamiri kwa wafugaji hawahawa tunaowalaumu kila kukicha endapo tu mfumo mzima wa uendeshwaji na usimamizi wa sera na sheria ukiwa sahihi. Tuhamasishe kilimo cha malisho kwa wafugaji, tutumie mashamba darasa kuelimishia wafugaji hakika kilio cha malisho msimu wa kiangazi tutakitokomeza.
MAKAMU M/KITI TRSA
Subscribe to:
Posts (Atom)




















