Friday, 14 July 2017

HEI (HAY) BORA NI IPI?

 Na, Floidin John Linus,     Email. floidinjohn@gmail.com

Wafugaji wengi hapa nchini wamekuwa wakikosa uhakika wa chakula cha mifugo kwa
Nyasi zikifungwa kuhifadhiwa
msimu(mwaka) mzima wa uzalishaji. Hii ni kutokana na kutegemea zaidi vyanzo asilia vyenye kuwezesha uwepo wa malisho na maji. Hata hivyo kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi, ongezeko kubwa la uhitaji wa mazao ya mifugo na ongezeko la watu, mfumo wa uzalishaji hauna budi kubadilika zaidi na kuwa wa kisasa. Kuweza kuendana na mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo kwa kiasi kikubwa yanaathiri ufugaji kutokana na upungufu wa malisho msimu wa ukame.
Kama nilivyowahi kuandika namna bora ya kuandaa shamba la nyasi HAPA ili kuweza kupata uhakika wa chakula cha mifugo. Hata hivyo baada ya kuvuna kama ilivyoelezwa katika LINK hapo ya kustawisha shamba la nyasi, mfugaji au mkulima anaweza kuhifadhi nyasi katika mfumo wa nyasi kavu au hei (hay). 
Kuvuna nyasi na kuzihifadhi kwa mfumo wa nyasi kavu ni bora zaidi kwa sababu huzuia upotevu wa chakula kwa kukanyagwa na kuchafuliwa hovyo na wanyama, badala yake mfugaji huweza kulisha kulingana na mahitaji.Hata hivyo kwa vile, hei ndio mfumo unaotumika zaidi kuhifadhi nyasi kwa ajili ya mifugo, mfugaji lazima atambue sababu zinazosababisha ubora wa hei pamoja na namna ya kutambua hali ya ubora wa hei aliyoitunza.

Hei iliyofungwa vizuri
Ubora wa hei haswa hutizamwa kwa kiwango cha virutubisho(nutrients) kilicho ndani ya nyasi hizo. Kiwango cha protini, nyuzi nyuzi (fiber content) na umengenywaji(digestibility) huweza kutumika kutambua ubora wa hei iliyohifadhiwa.
Hata hivyo kwa mfugaji wa kawaida hawezi kupata uwezo wa kufanya tafiti maabara kutambua ubora wa nyasi alizohifadhi. Hivyo anaweza kulinganisha ubora wa chakula(hei) kwa kuangalia kiwango cha uzalishaji cha mnyama anachotakiwa kuwa nacho, mfano kiasi cha maziwa na ongezeko la uzito. Ijapokuwa uzalishaji hafifu siyo tu sababu ya ukosefu wa lishe duni, kuna sababu nyingine pia kama hali ya hewa na magonjwa, hivyo majawabu ya maabara ni bora zaidi.
 Jambo la kuzingatia ni kwamba, hapo juu nimeongelea zaidi kutambua ubora wa hei kwa kuangalia hali ya mnyama zaidi. 

Tunapozungumzia ubora wa hei, unaweza ukasababishwa na vyanzo mbali mbali na kusababisha kuongezeka au kushuka kwa ubora wa hei inayozalishwa na mfugaji kwa ajili ya mifugo au biashara.

Shamba la nyasi
Sababu hizo ni kama vile,
  • Aina ya nyasi, nyasi hutofautiana kiwango cha virutubisho na madini kwa ajili ya mifugo. Pia vile vile uwezo wa kufyonza katika udongo na ukuaji wake.
  • Ukuaji wake, ubora wa hei hupotea haraka kadri nyasi zinavyozidi kukomaa. Hivyo mfugaji  hushauriwa kuvuna nyasi mapema kabisa baada ya kuanza kutoa maua.
  • Hali ya hewa na utunzaji wake,  mfano baada ya kuvuna mvua ikinyeshea nyasi husababisha upotevu wa virutubisho. Pia vilevile jua kali husababisha upotevu wa Vitamini A na kupukutika (kuvunjika vunjika) kwa majani.
  • Kiasi cha mbolea kwenye udongo, kiwango cha kutosha cha madini ya chokaa, nitrojeni, fosifeti (phosphate), Potassium (K) na madini mengine yanayohitajika kwa kiasi kidogo ni muhimu kwa ajili ya kuzalisha hei yenye ubora.
KILIMO CHA NYASI NI BIASHARA INAYOLIPA.

Thursday, 13 July 2017

NANI ATUSAIDIE ATEGUE KITENDAWILI HIKI?

By, Floidin John Linus,     Emai. floidinjohn@gmail.com

Katika jamii yetu ya kitanzania mtu anaposikia neno UFUGAJI au WAFUGAJI picha inayokuja kichwani kwanza ni NG'OMBE. Fikra ya kwanza haipeleki mawazo kwenye mbuzi, kondoo, nguruwe, sungura, kuku au mifugo mingine. 
Maana yake ni kwamba ufugaji katika jamii yetu unapeperushwa na nembo ya NG'OMBE. Tunaposikia serikali ikitangaza ongezeko la mapato kutokana na ufugaji, tunautizama mchango wa ng'ombe kwanza.
Lakini kujivuna kote kuhusu upatikanaji wa nyama, maziwa, ngozi na mazao mengine ya mifugo yanategemea wafugaji hawa waliojaa sehemu mbalimbali za nchi yetu katika mbuga wakichunga. Hata tunapotizama maduka ya nyama katika miji mbalimbali ni mchango wa wafugaji hawa hawa wa asili. 
Ufugaji sasa ni fursa kubwa sana kutokana na ongezeko kubwa la uhitaji wa mifugo pamoja na mazao yake mbalimbali. Kwa bahati nzuri au mbaya ufugaji wa nchini umeegemea zaidi kwa jamii kadhaa zilizo zoeleka tangu awali kama jamii za kifugaji.

Kutokana na fursa hii wafugaji wamekuwa wakitumia ufugaji wao kwa ajili ya kujipatia kipato chao kinachokidhi mahitaji yao ya kila siku. Changamoto lukuki zinazokabili ufugaji hapa hatuwezi kuzipuuzia hata kidogo katika kukwamisha maendeleo zaidi katika sekta hii ya mifugo.
Hivyo basi kutokana na uhitaji mkubwa  wa mifugo na mazao yake kuna namna mbili ambazo wafugaji wamekuwa wakitumia kuhakikisha wanafikia uhitaji wa soko na kukidhi mahitaji yao.
1. Kuongeza idadi ya mifugo   
2. Kuboresha mbinu za ufugaji.
1. KUONGEZA IDADI YA MIFUGO, hii ndiyo njia ambayo wafugaji wetu wa asili wamekuwa wakiitumia kuhakikisha kwamba wanafikia hitaji la soko pamoja na kulinda tamaduni (kijamii) zao.
Hata hivo haya mambo mawili yamekuwa na mchango mkubwa sana katika kusababisha ongezeko la mifugo hapa nchini. Ongezeko hili linatokana na changamoto za kibaiolojia na kimazingira zinazo sababisha uzalishaji hafifu wa mifugo ya asili hivyo wafugaji kuwalazimu kuongeza mifugo zaidi ili kupata mazao zaidi ya mifugo. Hata hivyo ongezeko hili limekuwa na madhara makubwa katika mazingira kutokana na uharibifu unaotokana na ardhi kushindwa kustahimili ongezeko hili. Mmomonyoko wa ardhi, uharibifu wa nyanda za malisho, vyanzo vya maji na huduma duni imekuwa ni changamoto kutokana na wingi wa mifugo. Sababu kama vile,
  • Mbegu duni za mifugo
  • Ukosefu wa elimu ya kutosha kwa wafugaji wetu
  • Mabadliko ya tabia ya nchi na
  • Serikali kutotimiza majukumu yake ipasavyo, ni baadhi tu ya mambo yanayosababisha mfumo huu wa wafugaji kutumika kuongeza uwezo wa kupata zaidi mazao yamifugo.
2. KUBORESHA MBINU ZA UFUGAJI, huu kwa bahati mbaya siyo mfumo tunaouona ukishamiri katika jamii tunazozitegemea kwa kiwango kikubwa katika sekta ya ufugaji.Umekuwa ni
mfumo unaoshamiri zaidi kwa wajasiriamali wanaowekeza katika ufugaji. Maana yake ni kwamba mfumo huu haujaweza kushawishi wafugaji wetu wa asili. Yawezekana kabisa kwamba nguvu inayotumika kushauri wafugaji haijakidhi mahitaji iongezewe nguvu ama haijaendana na uhitaji itafutwe njia mbadala. Katika jambo hili, serikali nayo inachuku nafasi kubwa sana kuzorotesha mfumo huu. Tukiangalia jitihada zilizofanyika wakati wa awamu ya kwanza na baada ya azimio la Arusha tunaamini kama zingeendelezwa basi leo hii tungeweza kuwa tunaongelea jamii za kifugaji zenye ufugaji wa kisasa. 
Huu ni mfumo ambao unaendana kabisa na mabadiliko ya dunia kwa sasa. Unaendana na hitaji la soko kwa kuzalisha mifugo na mazao yake bora kabisa kuweza kushindana katika masoko ya kimataifa. Lakini pia vilevile ni mfumo rafiki kwa mazingira. 
Mfumo huu unahitaji mabadiliko ya kifikra kwa wafugaji na nguvu ya serikali na wadau wa mifugo kuhakikisha tunatoka katika ufugaji wa asili na kuingia mfumo huu wa kisasa. 
Ni mfumo wenye gharama sana lakini matunda yake ni makubwa zaidi kwa mfugaji,jamii na taifa kwa ujumla.
Swali la kujiuliza, ni nani atutegulie kitendawili hiki?. Jitihada zipi zenye kuonekana na thabiti kutupa mwelekeo wa mabadiliko haya. Kumlaumu mfugaji kutobadilika haisaidii bali kumwekea mfumo wa kumwezesha ndiyo itasaidia, ,mfano, wataalamu wa kutosha, uwepo wa mbegu bora za ng'ombe, madawa, soko na malisho bora (mbegu). KITENDAWILI HIKI HAKINA MTEGUAJI KWA SASA. Hata serikali nayo inaingia kwa kusita sita, vyama vya wafugaji ni hafifu na hata wadau wa sekta hii wamejiweka pembeni na kutupia lawama kundi fulani. 
Ufugaji ni fursa kubwa sana kama kuna nia ya dhati.