Thursday, 27 April 2017

Kifo cha mzee wetu hakika ni pigo kwetu na wadau wa mifugo.


Sisi kama chama cha wanafunzi tunaosomea usimamizi na uendelezaji wa nyanda za malisho (TRSA), tunayo masikitiko makubwa sana juu ya kifo cha mzee wetu pia mwalimu wetu Mr. Protace. 

Aidha taarifa hizi zimetushtua sana maana mara ya mwisho ni tulipomuona katika maonesho ya kumbukumbu ya waziri mkuu wa zamani wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, marehemu Mh. Edward Moringe Sokoine pale katika viwanja vya Chuo cha Kilimo cha Sokoine (Mazimbu campus).

Tunatoa pole kwa wanafamilia wote waliokutwa na msiba huu, idara ya sayansi ya wanyama, malisho na samaki (SUA),  viongozi wa Chama cha Wadau wa Nyanda za malisho Tanzania (RST) na wadau wote walionufaika na ujuzi wa mzee wetu.

TRSA tunamuombea kwa mwenyezi  Mungu amrehemu mzee wetu.
Tangulia mzee wetu hakika uliyoyafanya ni mengi sana na ni makubwa mno. Daima ulijaribu kutujenga katika misingi ya kupenda kila tulichokuwa tukikifanya. Ulitamani kila ulichokijua nasi tukifahamu kila ulipopata nafasi ya kuongea nasi. Yawezekana jitihada zako za kutupa ujuzi wako ilikuwa ni ishara ya ukomo wa maisha yako hapa duniani hivyo ulihitaji usiondoke na deni la kutompatia yeyote aliyetamani kuonja ujuzi wako wa kitaalamu.

Nyuma yako ni mbele yetu hakika 
tunaomba mwenyezi Mungu akupumzishe salama.

Naamini siku moja tutakutana huko pia kwa

namna tofauti maana sote ni wapitaji hapa duniani.
Kile ulichotupatia nasi tutakitumia kuisaidia 

jamii kama ishara ya kuenzi urithi uliotuachia

vichwani mwetu.

Tunawaombea wote waliopatwa na msiba huu, haswa familia yake pamoja na ndugu na jamaa Mungu awatie uvumilivu na moyo wa ujasiri katika kipindi hiki kigumu.

Familia ya wana-TRSA na wahitimu wa shahada ya usimamizi na uendelezaji wa nyanda za malisho tuko pamoja nanyi katika wakati huu mgumu.

Bwana alitoa na Bwana ametwaa
jina lake lihimidiwe.



Imeandaliwa na makamu mwenyekiti TRSA
Linus, Floidin John.



Saturday, 8 April 2017

Sekta ya mifugo itupiwe jicho la tatu...


Ukisoma sera yetu ya mifugo ya mwaka 2006 bonyeza hapa inaonesha jinsi gani kama taifa tuna ndoto ya kufikisha sekta ya ufugaji katika mfumo mpya na wakisasa zaidi. Inatoa maelekezo na namna ya kuendana na kasi ya ukuaji wa kiuchumi n.k. Lakini bahati mbaya   tunatamani kufika katika mafanikio tusiyoyawekea nguvu na nia thabiti ya kuhakikisha tunatekeleza matakwa ya sera yetu na kufikia katika mafanikio tunayoyatamani.
Ni ukweli ulio wazi kuhusu msululu mkubwa wa faida zinazotokana na ufugaji. Yawezekana ufugaji unashindwa kuendelea sababu ya kufichwa nyuma ya pazia la kilimo. Pazia la kilimo kubeba ufugaji limekuwa kikwazo kwa maendeleo ya mifugo kuanzia ngazi ya serikali hadi kwa wananchi wa kawaida. Nasema hivi kwa sababu sekta ya kilimo na mifugo ni shughuli za kiuchumi ambazo kwa ujumla zinaenda pamoja. Na ndiyo maana hata Mheshimiwa Raisi John Pombe Magufuli akaamua kuziunganisha kuwa sekta moja. Lakini ufugaji umekuwa ukitembea chini ya kivuli cha kilimo. Tunashuhudia fursa nyingi zikirudi upande wa kilimo mfano, utoaji wa ruzuku, mikopo, mbegu za mazao (kilimo) hakuna mbegu za malisho, ardhi, masoko bora, mbolea, kilimo cha umwagiliaji n.k . Huduma sawa na zinazopelekwa kwenye kilimo tulitegemea pia zielekezwe kwenye kuinua ufugaji lakini ni tofauti kabisa.   Mchango wa ufugaji ijapokuwa ni mkubwa katika uchangiaji wa mapato ya halmashauri mbalimbali, mfano minada lakini  umekuwa hauleti mrejesho sawa na nguvu ya kuhakikisha uboreshwaji wa ufugaji unazingatiwa.

Sekta ya mifugo inakua kwa kasi ya kusuasua sababu ya ukosefu wa mipango madhubuti. Ukuaji wake unategemea zaidi  ukuaji wa kipato kwa mfugaji na taifa kwa ujumla ikisaidiwa na ukuaji  wa teknolojia na miundombinu.
Matatizo ya ukosefu wa teknolojia thabiti kama mbegu bora za ng'ombe wa maziwa na nyama yamesababisha kudunisha sekta hii ya mifugo hapa nchini. Lakini hatuwezi kupuuzia mchango wa mapungufu ya kisera na kisheria hapa nchini katika kuchangia kudolola kwa sekta ya mifugo.
Bahati mbaya zaidi serikali imeshindwa kuweka mazingira salama ya kuhakikisha ufugaji unanufaika na ongezeko la watu hapa nchini. Tunategemea ongezeko la watu liendane na uhitaji mkubwa zaidi wa mifugo na mazao yake hivyo lazima uzalishaji uongezeke zaidi, lakini je ni kweli hapa nchini Iko hivyo?
Tunashudia uharibifu mkubwa wa maeneo ya malisho sababu ya ongezeko la watu na kuvamia maeneo ya malisho kiholela, kilimo cha kuhama hama n.k. Wafugaji wanafuga kiholela na kimazoea sababu ya ukosefu wa elimu ya kutosha. 
Wafugaji wetu ni wafugaji wenye ufugaji wa kurithishana. Hivyo hata namna ya ushughulikiaji wa mifugo lazima uendane na namna alivyokua akiona wakubwa wake wakihudumia mifugo. Hatutegemei wafugaji kubadilika bila kuweka nguvu na jitihada za dhati kuwabadilisha. 

Yawezekana hata wataalamu wenyewe wakakata tamaa sababu ya wafugaji kutobadilika. Lakini haina budi kuzidi kuwasaidia maana ufugaji kwao ni utamaduni. Kupambana na utamaduni kuwarudisha kwenye mtizamo wa kiuchumi lazima kupambana nao taratibu.
Mahitaji ya wafugaji serikali iyaangalie upya kama mikopo, ruzuku kwenye madawa, mbegu za malisho n.k ili kuchochea ukuaji wa sekta ya mifugo. Sekta ya mifugo isitembee chini ya kivuli cha kilimo.
Niiombe serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, wadau na jamii kwa ujumla kushirikiana kumkwamua mfugaji. Lakini na wafugaji wetu wawe tayari kupokea mabadiliko haya.


IMEANDALIWA NA MAKAMU MWENYEKITI TRSA
Linus Floidin John.