Ukisoma sera yetu ya mifugo ya mwaka 2006 bonyeza hapa inaonesha jinsi gani kama taifa tuna ndoto ya kufikisha sekta ya ufugaji katika mfumo mpya na wakisasa zaidi. Inatoa maelekezo na namna ya kuendana na kasi ya ukuaji wa kiuchumi n.k. Lakini bahati mbaya tunatamani kufika katika
mafanikio tusiyoyawekea nguvu na nia thabiti ya kuhakikisha tunatekeleza matakwa ya sera yetu na kufikia katika
mafanikio tunayoyatamani.
Ni ukweli ulio wazi kuhusu
msululu mkubwa wa faida zinazotokana na ufugaji. Yawezekana ufugaji unashindwa
kuendelea sababu ya kufichwa nyuma ya pazia la kilimo. Pazia la kilimo kubeba
ufugaji limekuwa kikwazo kwa maendeleo ya mifugo kuanzia ngazi ya serikali hadi
kwa wananchi wa kawaida. Nasema hivi kwa sababu sekta ya kilimo na mifugo ni shughuli za kiuchumi ambazo kwa ujumla zinaenda pamoja. Na ndiyo maana hata Mheshimiwa Raisi John Pombe Magufuli akaamua kuziunganisha kuwa sekta moja. Lakini ufugaji umekuwa ukitembea chini ya kivuli cha kilimo. Tunashuhudia fursa nyingi zikirudi upande wa kilimo mfano, utoaji wa ruzuku, mikopo, mbegu za mazao (kilimo) hakuna mbegu za malisho, ardhi, masoko bora, mbolea, kilimo cha umwagiliaji n.k . Huduma sawa na zinazopelekwa kwenye kilimo tulitegemea pia zielekezwe kwenye kuinua ufugaji lakini ni tofauti kabisa. Mchango wa ufugaji ijapokuwa ni mkubwa katika uchangiaji wa mapato ya halmashauri mbalimbali, mfano minada lakini umekuwa hauleti mrejesho sawa na
nguvu ya kuhakikisha uboreshwaji wa ufugaji unazingatiwa.
Sekta ya mifugo inakua kwa kasi
ya kusuasua sababu ya ukosefu wa mipango madhubuti. Ukuaji wake unategemea
zaidi ukuaji wa kipato kwa mfugaji na
taifa kwa ujumla ikisaidiwa na ukuaji wa
teknolojia na miundombinu.
Matatizo ya ukosefu wa teknolojia
thabiti kama mbegu bora za ng'ombe wa maziwa na nyama yamesababisha kudunisha
sekta hii ya mifugo hapa nchini. Lakini hatuwezi kupuuzia mchango wa mapungufu
ya kisera na kisheria hapa nchini katika kuchangia kudolola kwa sekta ya
mifugo.
Bahati mbaya zaidi serikali
imeshindwa kuweka mazingira salama ya kuhakikisha ufugaji unanufaika na
ongezeko la watu hapa nchini. Tunategemea ongezeko la watu liendane na uhitaji
mkubwa zaidi wa mifugo na mazao yake hivyo lazima uzalishaji uongezeke zaidi,
lakini je ni kweli hapa nchini Iko hivyo?
Tunashudia uharibifu mkubwa wa
maeneo ya malisho sababu ya ongezeko la watu na kuvamia maeneo ya malisho
kiholela, kilimo cha kuhama hama n.k. Wafugaji wanafuga kiholela na kimazoea sababu ya ukosefu wa elimu ya kutosha.
Wafugaji wetu ni wafugaji wenye ufugaji wa kurithishana. Hivyo hata namna ya ushughulikiaji wa mifugo lazima uendane na namna alivyokua akiona wakubwa wake wakihudumia mifugo. Hatutegemei wafugaji kubadilika bila kuweka nguvu na jitihada za dhati kuwabadilisha.
Yawezekana hata wataalamu wenyewe wakakata tamaa sababu ya wafugaji kutobadilika. Lakini haina budi kuzidi kuwasaidia maana ufugaji kwao ni utamaduni. Kupambana na utamaduni kuwarudisha kwenye mtizamo wa kiuchumi lazima kupambana nao taratibu.
Mahitaji ya wafugaji serikali iyaangalie upya kama mikopo, ruzuku kwenye madawa, mbegu za malisho n.k ili kuchochea ukuaji wa sekta ya mifugo. Sekta ya mifugo isitembee chini ya kivuli cha kilimo.
Niiombe serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, wadau na jamii kwa ujumla kushirikiana kumkwamua mfugaji. Lakini na wafugaji wetu wawe tayari kupokea mabadiliko haya.
IMEANDALIWA NA MAKAMU MWENYEKITI TRSA
Linus Floidin John.
No comments:
Post a Comment