Thursday, 30 March 2017

KUSTAWISHA SHAMBA LA NYASI KATIKA NYANDA KAME.

             Chanzo; CHAMA CHA NYANDA ZA MALISHO TANZANIA (RST).
                             P.O.BOX 3004, CHUO KIKUU MOROGORO- TANZANIA.

Changamoto za kustawisha shamba la nyasi.
Mifugo katika machunga ya jumuiya
ü  Machunga mengi nchini ni ya jumuiya nani astawishe nyasi?
ü  Mifugo inaranda randa hovyo kwa hiyo ni vigumu kustawisha mashamba binafsi ya malisho
ü  Uhaba wa mbegu za malisho na utaalamu wa kustawisha malisho vijijini unadhoofisha ari ya kupanda malisho.



Kuongeza wingi wa mbegu za nyasi.
ü  Ili kuongeza wingi  wa mbegu za nyasi panda kitalu cha nyasi kwa kutumia vishina vya nyasi.
ü  Chimba kijaluba chenye kina cha sentimeta 40 na upana wa sentimeta 100 na urefu wa sentimeta 500.
ü  Weka ndoo 5 za samadi na mbolea ya kupandia (DAP) gramu 500.
ü  Halafu panda vishina vya nyasi sentimeta 25 X 25.

Kustawisha shamba la nyasi.

Kitalu cha nyasi kilichopandwa
ü  Chimba mitaro yenye kina cha sentimeta 40 kwa trekta au jembe la kukokotwa na ng’ombe; nafasi kati ya mitaro ni sentimeta 50.
ü  Changanya mbolea zote na udongo vizuri.
ü  Mvua inaponyesha na kukolea vizuri panda vishina vya nyasi toka katika kitalu cha nyasi.

Kutunza shamba la nyasi
Kitalu cha nyasi kilichostawi
ü  Palilia shamba la nyasi wiki la tatu na la sita baada ya kupanda.
ü  Weka mbolea ya kukuzia kilo 50 kwa ekari moja katika wiki la tatu baada ya kupanda.





Kuvuna shamba la nyasi.

ü  Vuna nyasi siku 84 baada ya kupanda kabla ya hapo mizizi inakuwa haijakua vizuri.
ü  Vuna nyasi kiasi cha sentimeta 15 juu ya ardhi. Vuna kila nyasi zinapotoa maua.

ü  Sambaza samadi, DAP kilo 50 na mbolea ya kukuzia kilo 50 kwa ekari kila mwaka mvua zinapoanza.

Shamba la nyasi lililostawi vizuri.




IMEANDALIWA NA MAKAMU MWENYEKITI TRSA
LINUS FLOIDIN JOHN.





Wednesday, 22 March 2017

MATUMIZI YA MABUA(STRAWS) KWA AJILI YA MIFUGO


N'gombe wakila mabaki ya mpunga.

Mabua ni mabaki yanayopatikana baada ya mavuno shambani. Haya yanaweza kuwa ni mabaki ya mpunga, mahindi, mtama , ngano n.k
Mfugaji hupitia changamoto mbalimbali ya upatikanaji  wa  malisho katika misimu tofauti tofauti haswa kutokana na tatizo la upatikanaji wa mvua pamoja na ardhi ya kutosha.

Hata hivyo wafugaji(pastoralists) wa kitanzania wameanza kujikita katika kilimo (agro-pastoralists) kwa ajili ya kujipatia chakula na kuuza kupata kipato pasipo kutegemea mifugo pekee(diversfication). Baada ya mavuno mabaki (mabua) yanayobaki shambani huweza kutumika kwa ajili ya mifugo.

Mabua uhusisha  shina na sehemu ya majani, hata hivyo mabaki haya yana kiasi kingi cha lignin (nyuzi nyuzi ngumu) pamoja na uchache wa virutubisho kwenye mabua.

Kwa mabaki ya mahindi, mabua(straws) na mabunzi(corns) huweza kutumika kwa ajili ya mifugo.



Lakini mabaki ya mpunga shina hutumika zaidi sababu ya ulaini wake wa kumengenywa(digestibility) kuliko majani yake.
Hata hivyo haya mabua huwa na changamoto ya kuliwa na kumengenywa kwa kiasi kidogo sana (poor digestibility and feed intake) na changamoto ya ukosefu wa virutubisho vya kutosha(low nutritive values). Kutokana na sababu hizi kumekuwa na njia mbalimbali za kuboresha haya mabua kuweza kuliwa kwa wingi zaidi na kuyaongezea baadhi ya virutubisho muhimu kwa mifugo. 

NJIA ZA KUBORESHA MABUA
Njia zitakazo orodheshwa hapa zitakuwa ni njia za kutumia kemikali pekee katika uboreshaji wa mabua kwa ajili ya mifugo.
  1. Kutumia NaOH, kumekuwa na mawazo tofauiti kutoka kwa wasomi mbalimbali kuhusu matumizi ya NaOH iliyoanzishwa na Beckmann. Haipatikani kiurahisi kwa wafugaji wadogo. Ni njia ambayo kemikali hii hutumika kuongeza umengenywaji(digestibility) na uliwaji wake(feed intake). Beckmann alisema mabua hulowekwa kwenye maji yenye kemikali kwa masaa 18-20 ijapokuwa baadae huoshwa kwa maji safi kisha kupewa wanyama. Njia hii ilionekana kuwa na mapungufu hivyo kufanyiwa marekebisho na Torgrimsby mwaka 1971, Wethje mwaka 1975 na baadae zikagundulika njia za kupulizia. Ni njia yenye changamoto ya kusababisha uchafuzi wa mazingira na kusababisha ongezeko la Na katika mazingira.                                                  
  2. Kutumia NH3, ammonia namna ya utumiwaji wake ni sawa na NaOH, Huongeza umengenywaji, huongeza nitrojeni na kuzuia kuvu. Ijapokuwa matumizi ya nitrojeni hayana matokeo mazuri kama NaOH lakini humsaidia mfugaji kupunguza gharama za vyakula vya mifugo kwa ajili ya nitrojeni.
  3. Matumizi ya UREA, 

        Urea hutoa amonia mara inapoyeyuka. Ipo         katika mfumo yabisi hivyoni rahisi                     kusafirishwa. Mabua hukatwa katwa kisha         kuchanganywa ama kupuliziwa na maji            yenye 2.5-5% ya urea. Yaani kilo 1 ya                mbolea ya urea (46% nitrogen)                       hukorogwa ndani ya lita 10 za maji. Kiasi         hiki cha maji hutumika kwa mabua yenye         uzito wa kilo 16 hadi 20. Kisha hufunikwa          kwa muda wa wiki 2 hadi 3. Hii ni njia ambayo hata mfugaji wa kawaida anaweza kutumia kwa ajili ya kuboresha hali ya mabua ili kuweza kupata nishati kubwa zaidi iliyo ndani ya mabua. Mfano wa jinsi ya kuandaa pia ni kama ilivyooneshwa hapa chini kwenye picha.

mabua yaliyoshughulikiwa vizuri huwa na harufu ya mkojo baada ya wiki 2-3.

Baada ya wiki hizo, unapofungua sehemu yalipoifadhiwa na kutoa chakula hicho cha mifugo basi kiache wazi kwa muda kabla ya kuwapa wanyama ili kuruhusu harufu kali ya ammonia kupungua. Chakula hiki pia huweza kutumika kwa ajili ya kunenepeshea (fattening) na kuongezea uzito wanyama.


 4. Kutumia mkojo, hii ni njia ambayo ni rahisi kutumia kutokana na upatikanaji wa mkojo wa wanyama wenyewe. Huweza kutumika sawa sawa kabisa na matumizi ya UREA hapo juu. Mkojo pia huweza kunyunyiziwa kama urea na kufata taratibu zile zile. Mkojo huzalisha UREA na AMMONIA. Hivyo huboresha umengenywaji(digestibility) na huongeza nitrojeni kwenye chakula-mabua. Changamoto kubwa ya kupata mkojo ni kutenganisha kinyesi cha wanyama na mkojo. Hivy njia hii huonekana si salama sababu ya mazingira ya kupata mkojo.

5. Kunyunyizia chumvi chumvi au molasi, hii itaongeza hamu zaidi ya wanyama kula chakula kingi zaidi kutokana na chumvi chumvi au molasi kunyunyiziwa kwenye mabua.



IMEANDALIWA NA MAKAMU MWENYEKITI WA TRSA
Linus Floidin John.


Monday, 20 March 2017

UMUHIMU WA MTI WA MLUSINA KATIKA UFUGAJI.

Leucaena leucocephala
Kwa jina la kisayansi unaitwa Leucaena leucocephala.
Kwa kiingereza huitwa Leucaena au Lead tree.
Kiswahili huitwa mti wa Mlusina.

Mmea huu jamii ya mikunde(leguminous) asili yake ni Mexico. Lakini hapa nchini pia hustawi vizuri kabisa. Ni kati ya miti yenye jamii ya mikunde inayokua kwa haraka sana. Ni chanzo cha chakula kwa mifugo . Hupandwa pembeni ya shamba kama kuonesha mpaka wa shamba, kutoa kivuli, kizuia upepo(wind breaker), kuzuia mmomonyoko wa ardhi au maalumu kwa ajili ya chakula cha mifugo. Mti huu ukiachwa kwa takriban mwaka 1.5 huruhusu mzizi mkuu kuingia ndani zaidi ya udongo hivyo  kuhakikisha uzalishaji wa chakulacha mifugo hata wakati wa kiangazi kipindi ambacho hakuna chakula cha kutosha au ubora wa malisho unapokuwa mbovu.

Shina laini na majani yake ni chanzo kizuri cha protini kwa mifugo na virutubisho vingine kama carotenoids na  vitaminslakini pia huambatana na asidi-amino iitwayo mimosine ambayo huwa  na athari endapo chakula kinachotokana na jamii hii ya mikunde kitatumiwa pasipo uangalifu, haswa wanyama wenye tumbo moja(monogastric) kama nguruwe, kuku na sungura huathirika zaidi na huweza kusababisha kifo kwa wanyama hawa.

Mlusina hufananishwa na mkunde mwingine (alfaalfa) muhimu kwa wingi wa virutubisho haswa protini kwa ajili ya mifugo. Lakini  Mlusina una upungufu wa sodium na iodine lakini una wingi wa b -carotene.

                                         MAANDALIZI YA MLUSINA KWA AJILI YA MIFUGO
Majani ya mlusina yaliyoandaliwa kama chakula cha mifugo

Maandalizi ya mlusina kwa ajili ya chakula cha mifugo huandaliwa kwa kuondoa majani pekee kutoka kwenye matawi ya mlusina. Ni kwa sababu ndiyo sehemu ya mmea huu yenye kuwa rahisi zaidi kutumiwa na mifugo(digestible and palatable). Shina (stem) nalo huweza kutumika lakini labda sehemu changa kabisa kwa sababu ya changamoto ya tannins.

Majani haya hukaushwa juani ili kudhibiti madhara yatokanayo na asidi-amino ya mimosine ambayo ina athari kwa mifugo. Baada ya majani kupoteza kiasi cha maji ilichobeba, huwa tayari kwa ajili ya kuendelea na taratibu zingine za kuandaa chakula cha mifugo.

Majani ya Mlusina yaliyokaushwa

Chakula  kilichoadaliwa kwa ajili ya kuku huwekewa 5% ya majani ya mlusina, chakula kwa ajili ya nguruwe kinatakiwa kuwa na 10% tu ya mchanganyiko wa majani ya mlusina na chakula kinachoandaliwa kwa ajili ya ng’ombe kinatakiwa  kisichukue zaidi ya 30% ya mchanganyiko wa majani ya mlusina (Dongjing na Guodao, 1994).

Mlusina ni mzuri kwa sababu unapunguza gharama za kununua chakula cha kurutubishia mifugo(concentrates).


Hata hivyo, makala hii inajikita kwa matumizi ya Mlusina kwa ng'ombe. Maandalizi ya chakula kwa ajili ya ng'ombe yanatakiwa yasizidi 30%. Mfano kama chakula kinachoandaliwa ni kilo 100 maana yake ni kwamba majani ya Mlusina ambayo ni chanzo cha protini yanatakiwa yasizidi  kilo 30. Hata hivyo athari nyingi huonekana endapo asilimia za Mlusina zitazidishwa kwa kipindi kirefu, athari hizo ni kama vile kunyonyoka nywele(alopecia), matatizo katika ulaji(anorexia), kupoteza uzito, kutokwa na ute mdomoni(deep salivation), kuchubuka utumbo(esophagus lesions), kupoteza seli kwenye rumen na reticulum (necrotic papillae in the
rumen and reticulum), kuvimba kwa tezi (thyroid hyperplasia), kiasi kidogo cha homoni ya thyroxine(T4) kwenye damu, kifo cha kiinitete na vifo vya kabla na baada ya kuzaliwa (early embryonic mortality and perinatal death)  (Allison et al., 1992; Al-dehneh et al., 1994).

Ni vema mfugaji akawa na huu mmea ndani ya shamba lake kwa ajili ya mifugo yake kupata protini kwa wingi bila kutumia fedha nyingi kugharamia vyakula vya protini vinavyouzwa kwenye maduka mbalimbali ya vyakula vya mifugo.





IMEANDALIWA NA MAKAMU MWENYEKITI TRSA
Linus Floidin John.



Sunday, 19 March 2017

UVUNAJI WA MAJI MAENEO YENYE CHANGAMOTO YA UKAME NI UKOMBOZI WA UFUGAJI.


Mfumo wa kuvunia maji yanayotiririka.
Uvunaji wa maji (rain water harvesting) ni teknolojia inayotumika kukusanyia na kutunzia maji kwa ajili ya shughuli mbalimbali. Hata hivyo kuna njia nyingi au aina tofauti za uvunaji wa maji. 

Hata hivyo makala ya leo ni kutoa mtizamo wangu kwa wafugaji wa kitanzania(pastoralists) wanaoishi ama kufanya shughuli za ufugaji katika mikoa yenye changamoto ya ukame, mfano Dodoma, Manyara, Singida, Shinyanga na baadhi ya maeneo ya Morogoro.

Wafugaji wa kitanzania wamekuwa wakiathiriwa sana na tatizo la uchelewaji wa mvua za vuli. Husababisha ukosefu wa malisho na maji kwa ajili ya mifugo na wafugaji wenyewe. Aidha, kutotabirika kwa mvua pamoja na kiwango kidogo cha mvua ni changamoto katika shughuli ya ufugaji hapa nchini. 
Katika msimu wa ukame wafugaji wamekuwa wakihama kutoka sehemu moja hadi nyingine kuhakikisha kwamba wanapata mahitaji ya mifugo yao kama vile malisho na maji. Hata kama sehemu wanazoishi zina nyasi bado hulazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta maji kwa ajili ya mifugo. Kuhama hama kumekuwa kukisababisha hasara nyingi sana kama vile, migogoro ya mara kwa mara, uharibifu wa vyanzo vya maji, kupoteza muda mwingi ambao nguvu kazi ingetumika kufanya shughuli nyingine za kimaendeleo, kukosesha haki watoto ambao wana umri wa kwenda shule, uzalishaji hafifu wa mifugo sababu mifugo hutumia nishati kubwa sana kusafiri umbali mrefu hivo kupunguza ufanisi wa kushika mimba, ukuaji na uzalishaji wa maziwa na nyama iliyo bora zaidi.

Hata, hivyo wafugaji wetu wanaweza kutumia teknolojia mbadala ya kuvuna maji wakati wa masika na kuyatunza hadi msimu wa ukame kipindi ambacho kuna changamoto ya maji. Kiasi kikubwa cha maji wakati wa msimu wa mvua hutiririka juu ya uso wa dunia (surface run-off) na kusababisha matatizo makubwa kama mafuriko, mmonyoko wa ardhi na uharibifu wa miundombinu.

Eneo lililoathirika na mafuriko
Matatizo haya yamekuwa yakitokana na uwanda mkubwa unaokuwa tambarare na wenye ukosefu wa uoto wa kutosha kuzuia madhara ya maji yanayotiririka kwa kasi. Hata hivyo hatuwezi kupuuzia changamoto ya ubovu wa miundo mbinu katika kuchangia tatizo la mafuriko haya.

Wafugaji wana uwezo mkubwa sana wa kutumia fursa ya mvua inayonyesha ndani ya muda mfupi kwa mwaka katika maeneo yao kwa ajili ya kupambana na chanagamoto zinazosababishwa na ukame kwa upande wa ufugaji. Ni dhahiri kabisa, suala la mabadiliko ya tabia ya nchi linaathiri kila sekta hapa nchini. Hivyo basi, hata serikali tunayoitegemea ina kazi kubwa kupambana na mabadiliko haya kwa sekta zote. Lakini suala la uvunaji wa maji bado wafugaji wanaweza kulifanya kwa ufanisi mkubwa pasipo kuhitaji msaada wa kifedha kutoka serikalini labda tu ushauri wa kitaalamu pekee. Wafugaji wana hazina kubwa, mifugo ni hazina iliyobeba utajiri wa wafugaji. Wanatakiwa kujifunza kutokana na hasara kubwa wanayopata kila mara tunapokumbana na hali ya ukame hapa nchini. Kuna njia rahisi za kuvuna maji bila kutumia vifaa na zana za gharama kubwa kuandaa eneo la kuvunia maji. Kwa hazina ya mifugo waliyonayo wafugaji si jambo kubwa wala gumu kutumia hata teknolojia za asili (local technology) kuandaa eneo la kuvunia maji yatirirkayo msimu wa mvua.


Teknolojia ya asili ya kuvunia maji

 Hizi ni baadhi ya picha zinazoonesha teknolojia rahisi kabisa ya kuvunia maji na kuyatunza kwa ajili ya kutumia katika msimu wenye changamoto ya maji.

Huweza kufanywa kwa kufata mkodo au mteremko wa uelekeo wa maji lakini pia kama eneo linabeba kiasi kikubwa cha maji njia ya kuhamisha(divert) baadhi ya kiasi cha maji kuelekea eneo la kuvunia huweza kutumika pia.

Teknolojia ya asili ya kuvunia maji


 FAIDA ZA KUVUNA MAJI.
Faida za kuvuna maji ni nyingi sana,lakini ntajaribu kuorodhesha baadhi tu,
  • Kunyweshea mifugo msimu ambao maji hayapatikani ndani ya eneo husika kutoka kwenye vyanzo vingine.
  • Matumizi ya nyumbani kwa ajili ya familia.
  • Kumwagilizia malisho kama mfugaji ataamua kuzalisha malisho kwa ajili ya mifugo yake, hivyo kuhakikisha uwepo wa chakula cha mifugo.
  • Kupunguza tatizo la mmomonyoko wa ardhi.
  • Kupunguza tatizo la mafuriko kama kiasi kikubwa cha maji kitavunwa ili maji yasipotee bure.
  • Kuboresha hali ya ufugaji, sababu mifugo haitosafiri umbali mrefu kutafuta maji hivyo nguvu kubwa ya mnyama itaelekezwa kwenye ukuaji na uzalishaji.
  • Kupunguza tatizo la migogoro na watumiaji wengine wa ardhi.   


IMEANDALIWA NA MAKAMU MWENYEKITI TRSA
Linus Floidin John.

Saturday, 18 March 2017

KILIMO CHA MALISHO NI MUHIMU SANA KWA UFUGAJI WENYE TIJA

Gwatamala
Kitaalamu nyasi hizi huitwa  Tripsacum laxum.
Kwa kiingereza huitwa Guatemala grass.
Na kiswahili chake hujulikana kama   nyasi aina ya Gwatemala.
Asili yake ni kutoka nchini Mexico. Ni nyasi ambazo hudumu kwa muda mrefu(perennial), Huota na kukua kwa kusimama(erect) kwa urefu wa mita 2-3.
Huchomoza matawi kutoka kwenye vinundu(nodes) vya juu.





Hupandwa kwa kutumia vishina katika kipindi cha mwanzo wa msimu wa mvua.
Mfano wa vishina , kushoto ndiyo mfano wa kishina kilichoandaliwa kupandwa.

Hupandwa ndani ya mashimo ambayo yanakuwa umbali wa sentimita 50-65 kati ya shimo na shimo ili kutoa nafasi ya kutosha baina ya nyasi. Hupandwa katika mistari na kati ya mstari mmoja na mwingine iwe ni mita 100.
Mfano wa jinsi ya kupanda vishina  vya gwatamala.
Mfugaji anaweza kuandaa shamba na kupanda nyasi za gwatamala kwa ajili ya mifugo. Mahitaji ya kilimo hiki ni kwenye udongo wenye rutuba, Gwatamala huitaji  400 kg nitrogen, 80 kg phosphorus, 50 kg potassium, 50 kg calcium na 50 kg za magnesium kwa mwaka kwa hekta (Risopoulos, 1966).

Ijapokuwa nyasi hizi hupendelea sehemu zenye mvua ya kutosha lakini pia huweza kukua vizuri katika maeneo yenye udongo mzuri yanayopokea mvua kwa wastani wa 600mm kwa mwaka. Na wakati wa kiangazi hupunguza uwezo wa kuzalisha malisho. Hustahimili ardhi yenye asidi na aluminium lakini nyasi hizi hazistahimili maeneo yenye tatizo la kukumbwa na mafuriko.

Nyasi huweza kuwa tayari kuvunwa miezi sita baada ya kupandwa lakini huchukua tofauti ya miezi minne tu  kuvunwa msimu kwa msimu.

Ni nyasi nzuri kwa ajili ya ng'ombe wa maziwa kwa kukata na kulisha (green chop-chop for zero grazing) lakini pia nyasi za gwatamala zinaweza kutunzwa kwa mfumo sileji kwa ajili ya matumizi ya baadae katika msimu wa kiangazi.


IMEANDALIWA NA MAKAMU MWENYEKITI TRSA
Linus Floidin John.


Friday, 17 March 2017

UKIJALI ARDHI (MACHUNGA) UTAJALI MIFUGO PIA

MIFUGO IKIWA MACHUNGANI
Stocking rate ni idadi ya mifugo inayoweza kuchungwa ndani ya eneo fulani kwa muda maalumu. Hii ni muhimu sana kwa sababu inahakikisha hali salama ya ardhi na ufanisi(uzalishaji) wa mifugo hivo ni chanzo cha faida(kipato) ya ufugaji pamoja na kuyapa malisho uwezo wa kurudi katika hali yake ya awali(resilience). Idadi ndogo ya mifugo kwenye machunga ni  nzuri si tu kwamba inadumisha hali ya usalama wa udongo lakini pia ni njia sa kurekebisha eneo lililoathiriwa(poor land condition).  
Kwa kawaida hali ya udongo huwa mbaya kiuzalishaji endapo malisho yatatumika (utilization) kwa zaidi ya 30%. Hapa namaanisha uzito (weight) wa jani(grass) ni 100% hivyo basi ikipotea kuanzia 70% ndiyo hatari inayomaanishwa.


Idadi ya mifugo(stocking rate) inatakiwa isizidi au kuwa sawa na uwezo wa ardhi (carrying capacity) kuhudumia mifugo. Hii itasaidia mimea kuendelea kuzalisha(photosynthesis), kuimarisha hali ya udong(soil stability), ulinzi wa mfumo wa maji(watersheds) na kukidhi mahitaji ya viumbe vingine kama wadudu(insects) na wanyama pori(wild animals).

Mahitaji makubwa ya mifugo ni maji na malisho, mahitaji haya hubadilika sana ndani ya mwaka kutokana na sababu mbalimbali kama vile ukame n.k. Hata hivyo mahitaji ya mfugaji ni kuhakikisha kuwa shughuli yake ya ufugaji inatanuka zaidi ili kumpatia kipato zaidi. Hivyo kutokana na sababu nyingi zilizo nje ya uwezo wa mfugaji kama vile ugumu wa upatikanaji wa mbegu bora zenye kuzalisha kiwango kikubwa cha nyama au maziwa, 
NG'OMBE WA NYAMA AINA YA BONSMARA
mfugaji hulazimika kutumia mbegu za asili(ng’ombe) zenye vinasaba hafifu katika uzalishaji na ukuaji, lakini hapa huitajika kuwa na idadi kubwa zaidi ili kukidhi mahitaji.
NG'OMBE WA ASILI
 Ikumbukwe kwamba, ufugaji wa kitanzania kwa zaidi ya 90% ni ufugaji huria wenye kutegemea maeneo ya machunga ya jamii (communal grazing area) yasiyoendelezwa kujipatia malisho. Maeneo haya yamekuwa yakivamiwa na idadi kubwa ya mifugo (overgrazed) na kusababisha uharibifu mkubwa kama mmomonyoko wa udongo, makorongo, uvamizi wa magugu ndani ya malisho, uwepo wa mimea vamizi haswa isiyopendelewa na mifugo(undisarable species), vichaka na hatimaye uzalishwaji hafifu wa mifugo na mazao yake kutokana na ukosefu wa malisho ndani ya eneo husika. Na madhara haya husababisha mimea inayopendelewa na mifugo (desirable species) kupungua sana ndani ya machunga. Lakini kwa vile ndiyo mimea inayopendelewa zaidi na mifugo, hutumiwa sana(highly grazed) na mifugo na kusababisha matumizi yasiyokuwa na mlingano(poor grazing distribution & uneven grazing) ndani ya machunga na kusababisha uwepo wa vipara. Vipara ni matokeo ya mimea kushambuliwa kila mara inapojaribu kurudi hali yake ya awali( resilience) hata hivyo hutumiwa na mifugo kabla ya kufikia hali hiyo.

Kutokana na hizi changamoto za machunga ya jumuiya ni changamoto kusimamia idadi ya mifugo katika eneo husika haswa kwa kuzingatia ufugaji wa kuhamahama, machunga hupitia misimu ya kuelemewa na mifugo na misimu ya kupungua mifugo kutokana na uwepo wa malisho na /maji.
Lakini ni muhimu kuelewa uwezo wa ardhi kuzalisha malisho. Hii inaweza kutathiminiwa kwa kutumia kiwango cha malisho(standing crop end of growing season) mwanzo wa msimu wa kiangazi.
Tabia hatarishi ndani ya machunga zinazotokana na idadi kubwa lazima zifatiliwe ili kuzigundua mapema na kudhibiti idadi ya mifugo. Idadi ya mifugo ndani ya machunga lazima idhibitiwe ili kulinda ikolojia na ardhi iweze kuhudumia mifugo kwa ufanisi mkubwa.


IDADI YA MIFUGO INAWEZA KUKADIRIWA KWA HATUA KUU NNE.

4-step Procedure outlined by Holechek (1988)
  1. Calculate total usable forage
  2. Adjust total usable forage
  3. Calculate forage demand
  4. Balance supply/demand to stocking rate

Only useful to get a “guess” of initial stocking rat

Hatua hizi zitajadiliwa wakati mwingine…..


                               IMEANDALIWA NA MAKAMU MWENYEKITI TRSA.

KUUZA MIFUGO ISIONEKANE KAMA TU NDIYO NJIA PEKEE YA KUKABIRI MSONGAMANO WA MIFUGO KWENYE MAENEO YA MACHUNGA.

ARDHI ILIYOATHIRIWA NA SHUGHULI ZA UFUGAJI
Hapa lazima tuoneshe utofauti wa mtaalamu wa usimamizi na uendelezaji wa nyanda za malisho na wataalamu wengine.
Ni kweli ndani ya nchi yetu tunakabiriwa na maeneo yenye kuathiriwa na mikusanyiko ya mifugo eneo moja na kusababisha uharibifu wa mazingira na migogoro. Mikusanyiko hii chanzo chake ni katika hatua za utafutaji wa malisho, maji, kukimbia magonjwa ya mifugo na sababu zingine za kijamii. 

Mikusanyiko hii imeathiri ardhi na kusababisha mmomonyoko wa ardhi na makorongo, uharibifu wa vyanzo vya maji, migogoro ya mara kwa mara na uharibifu wa malisho.
Hata hivyo mikusanyiko hii imeonekana kuzidi kuongezeka kadri siku zinavyokwenda maana yake ni kwamba wafugaji wetu wanakumbana na changamoto nyingi machungani.

Ukisikiliza majadiliano ya watu wengi wanasema kuwa wafugaji wanatakiwa kutambua kuwa sasa ardhi imekuwa na matumizi mengi lazima wajifunze kutulia sehemu moja na kuzalisha kitaalamu na kisasa zaidi. Ni kweli lakini mabadiliko haya yanapofanyika wahusika wakuu hawaangalii mbadala wa wafugaji waliokuwa wanatumia maeneo haya, hatimaye hutoa nafasi ya wafugaji kutangatanga.
Mfugaji anakabiliwa na marekebisho ya matumizi ya ardhi yasiyojali mazingira rafiki ya shughuli yake. 

Ufugaji  unaonekana kama shughuli inayostahili kufanyiwa kwenye maeneo yasiyofaa kwa kilimo(remote & unproductive areas), lakini binafsi hii hoja huwa naipinga kwa sababu kuu mbili,
1)Tukisema ufugaji ufanyike katika maeneo yasiyofaa kwa kilimo, swali ni Je,katika karne hii yenye teknolojia za juu sana ni eneo gani lisilofaa kwa kilimo?. Mfano, teknolojia za umwagiliaji,mbegu bora za nafaka na mbolea.
2) Mahitaji ya malisho ni sawa kabisa na mazao ya nafaka, mfano mbolea ya kutosha na maji, vyote hivi hutimiza mahitaji ya mwili wa mnyama ili kufikia uzalishaji wenye tija zaidi na bora kwa mtumiaji.


Kwa kiwango kikubwa misongamano au mikusanyiko hii inasababishwa na watumiaji wengine wa ardhi wasiotoa mbadala wa mfugaji kupata mahitaji yake.
Mfano,
ü  Kumzuia mfugaji kuharibu vyanzo vya maji ni vizuri sana, lakini kumzuia mfugaji pasipo kumtengenezea njia mbadala ya kunyweshea mifugo yake pasipo kuathiri vyanzo vya maji ni mbaya zaidi.
ü  Kumwondosha mfugaji katika ardhi yenye rutuba ili kupanua shughuli za kilimo ni vema lakini kumwondosha bila kumwandalia sehemu nyingine yenye mahitaji stahiki ni kumwonea.
ü  Kumwondoa mfugaji ili apishe uwekezaji ni vema kwa uchumi wa nchi, lakini hatari ni pale asipoandaliwa eneo zuri la kuhamishiwa.
ü  Upanuzi wa maeneo tengefu(reserves) kwa ajili ya mapori na wanyama pori ni vizuri lakini unapomuondosha eneo husika unamtengenezea mbadala gani?
ü  Kukabidhi mamlaka ya vijiji kutenga maeneo ya malisho, ni vizuri lakini watu hawa wana elimu ya mifugo na wanajua ni maeneo gani na yenye sifa gani yanafaa kwa ajili ya mifugo?
Hiyo yote ni baadhi ya mifano inayosababisha mikusanyiko mikubwa ya mifugo kutokana na kukimbia sehemu mbalimbali zenye changamoto. Hivo ni ukweli kwamba kwa asilimia kubwa misongamano hii inasababishwa na watumiaji wengine wa ardhi japo mfugaji ndiye anaonekana tatizo.


            KUPUNGUZA  WINGI WA MIFUGO ENEO MOJA BILA KUUZA MIFUGO.
Hapa ndipo mtaalamu wa malisho anaweza kutofautiana na maamuzi ya wataalamu wasio wa machunga wasiojua sifa za mifugo kwenye machunga(grazing behavior).
Ø  Miundombinu ya maji, hii inaweza kuwa suluhisho la misongamano na kupunguza mikusanyiko ya mifugo kwenye machunga pasipo kuuza mifugo. Kupangilia umbali wa vituo vya maji(water sources) kulingana na aina ya mifugo iliyopo ndani ya machunga.Hii itasaidia kupunguza msongamano.
Ø  Kubadilisha maeneo ya kuchungia kufatana na umri, breed na spishi(species). Mfano, ndama wanaweza kuchungiwa maeneo yenye makorongo, mteremko mkali (rough terrain) hii pia itapunguza msongamano.
Ø  Kuwa na spishi tofauti ya mifugo hii itasaidia mifugo ya spishi tofauti kuweza kutumia aina tofauti ya aina ya mimea na maeneo tofauti.
Ø  Kagua eneo la machunga yawezekana msongamano wa malisho unasababishwa na uvamizi wa vichaka, mimea vamizi, magonjwa au wadudu hatarishi kama ndorobo n.k.

Utaalamu wowote ndani ya machunga ni vyema ukatizama kuongezea ardhi uwezo wa kuhudumia mifugo mingi zaidi ili kustawisha ufugaji hapa nchini.

                                        IMEANDALIWA NA MAKAMU M/KITI TRSA

Tuesday, 14 March 2017

TUJADILI KIDOGO KUHUSU NDOROBO (TSETSE FLY) TANZANIA.

Ndorobo ni wadudu warukao ambao husambaza trypanosomes wasababishao magonjwa ya trypanosomiasis na nagana kwa mifugo na malale kwa binadamu. Kwa Tanzania trypanosomiasis ni kati ya magonjwa yanayoathiri binadamu na mifugo. Ndorobo wana madhara mengi sana kwa mifugo kama vile kuongezeka kwa vifo, mimba kutoka, kushuka kwa uwezo wa kuzaliana, ukuaji hafifu, uzalishaji hafifu wa nyama na maziwa, kuzuia matumizi ya machunga,kuongeza gharama za kuzuia ndorobo n.k. Kwa Afrika inakadiriwa kuwa ni kilomita za mraba milioni 10 zenye ndorobo ambapo kati ya hizo ni takribani kilomita za mraba milioni 7 zinazostahili kwa kulishia mifugo na eneo lililobaki likiwa ni misitu. Ni 40% ya eneo la Tazania lililoathiriwa na ndorobo ambalolingefaa kwa shughuli za kilimo na kuchungia mifugo. Aidha anasema ni takribani mifugo milioni 4.4 na watu milioni4 ambao wako kwenye nafasi kubwa ya kuambukizwa ugonjwa unaotokana na ndorobo. Inakadiriwa kuwa ni takribani US$ 7.98 milioni zinapotea kila mwaka kutokana na madhara yatokanayo na ndorobo (Malele,2011). Kwa kiasi hiki cha pesa inatoa nafasi kubwa kutafakari ni kwa jinsi gani taifa na wafugaji wanapoteza mapato kama tu ndorobo wangedhibitiwa. Tanzania inakadiriwa kuwa na spishi(species) kumi (10) za ndorobo ambazo zimetapakaa kulingana na uwezo wa kila spishi kustahimili eneo husika. Aidha inaelezwa kuwa, kubadilika kwa matumizi ya ardhi, ongezekola watu na shughulu zinazohusu binadamu ni kati ya vyanzo vya kusambaa kwa ndorobo hapa nchini.

NJIA ZA KUDHIBITI NDOROBO

.
1. Kuondoa vichaka. Hii ni njia iliyoanza kutumika tangu enzi za ukoloni. Ilihusisha kuondoa aidha vichaka vyote au sehemu tu ya vichaka iliyoonesha kuwa kivutio ama makazi ya ndorobo. Kwa upande wa mazingira si rafiki sababu husababisha eneo kuwa wazi hivo kuwa na madhara mengi. Hivo haitumiki sana ijapokuwa inaweza kutumika kwa kuzingatia usalama wa mazingira. 2.

2. Kutumia kemikali

Hii ni njia ya kutumia dawa ya kuulia wadudu ambapo inaweza kupuliziwa kutoka angani(aerial spraying) kwa kutumia vifaa maalumu ama kupuliziwa kutokea ardhini(ground spraying), kila njia ina madhara yake na faida zake na viumbe vingine pia huweza kuathirika kutokana na kemikali inayotumika kuua ndorobo.Kemikali zinazoweza kutumika ni Dieldrin (a residual organochloride), Endosulfan (Thiodan; a non-residual organochloride) na Synthetic pyrethroids.

3. Sterile male release technique

Hii ni njia inayotumika kwa kuandaa madume ya ndorobo ndani ya maabara.Madume haya huondolewa uwezo wa mbegu zake kutungisha halafu huachiliwa kwenye eneo liliothiriwa na ndorobo. Ni njia ya gharama sana. Ijapokuwa kutokana na (Bonomi et al., 2011),G. fuscipes ina onekana kuwa tofauti katika njia hii. Njia hufanya ufanisi zaidi kama eneo linalokusudiwa ni dogo pia idadi ya madume yaliyo ondolewa uwezo wa kutungisha maabara yanatakiwa kuwa na idadi kubwa kuliko madume yaliyoko eneo husika.

4. Kutumia mitego

Hutengenezwa kwa kutumia kitambaa cheusi na bluu. Rangi nyeusi huwavuta ndorobo na kutua kwenye rangi nyeusi hivyo kuweza kuvutwa kwenye kifaa cha kukusanyia au sehemu ilikopakwa kemikali ya kuua ndorobo. Lakini pia kemikali za kuwavutia kama acetone, mkojo wa ngombe au mbogo huweza kutumika sababu hutoa harufu ya kuwavuta. Kuzingatia, kuna mitego ya aina nyingi kulingana na aina(spishi) ya ndorobo.

Hizo ni baadhi ya njia za kudhibiti ndorobo ambazo hutumika katika maeneo yaliyo athirika na ndorobo.

IMEANDALIWA NA MAKAMU M/KITI TRSA

Tuesday, 7 March 2017

TUJIFUNZE KULINGANA NA MAKOSA.

Huu ulikuwa ni mwaka ulioacha simanzi kubwa baina ya wafugaji ama jamii zinazotegemea shughuli ya ufugaji kwa ajili ya kuendeshea maisha yao. Simanzi hii imesababishwa na kuchelewa kwa mvua kulikosababisha kukosekana kwa malisho na maji kwa kiasi kikubwa hapa nchini na takribani ukanda wetu wote wa Afrika mashariki. Ni ukweli usiopingika kwamba madhara yatokanayo na uchelewaji wa mvua za vuli si mara ya kwanza kuyashuhudia hapa nchini. Kumekuwa na upotevu wa idadi kubwa ya mifugo inayokufa sababu ya ukosefu wa malisho na maji ndani ya msimu wa kiangazi. Lakini swali ni moja kwamba NI KWELI TUNAJIFUNZA KUTOKANA NA MAKOSA?. Hapa hakuna wa kulaumiwa kuhusu mabadiliko ya tabia ya nchi lakini alaumiwe yule mwenye uwezo wa kufikisha elimu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi. Katika nchi yetu kuanzia wasomi na hata wale wasio na elimu ya darasani swala la kilimo cha malisho ni wimbo usioeleweka masikioni mwao. Lakini je, tuache kuchukua njia sahihi kwa sababu ya ukosefu wa uelewa juu ya swala hili? Kilimo cha malisho ndio njia pekee ya kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi. Ni njia itakayomwezesha na kumuhakikishia mfugaji uhakika wa chakula cha mifugo wakati wa kiangazi. Mfugaji mwenye kuweza kudhubutu kulima malisho atakuwa na uwezo wa kuvuna na kuweka akiba ya malisho(kipindi cha msimu wa masika) na kutumia akiba hiyo kipindi cha kiangazi wakati ambapo kuna upungufu mkubwa wa malisho. Jukumu hili linabaki kwenye mamlaka husika kuhakikisha mbegu za malisho bora zinapatikana ili elimu ya kilimo malisho iambatane na mbegu za malisho. Katika kipindi hiki ambacho mifugo mingi inakufa tusiwalaumu wafugaji kwa kuwaambia hawataki kuuza mifugo haswa msimu wa kiangazi wakati tunajua mapungufu ya soko letu la mifugo na mazao yake. Tusiwalaumu kutangatanga wakati tunajua hali ya machunga hapa nchini. Tunao uwezo wa kukomboa ufugaji na ukaendelea kushamiri kwa wafugaji hawahawa tunaowalaumu kila kukicha endapo tu mfumo mzima wa uendeshwaji na usimamizi wa sera na sheria ukiwa sahihi. Tuhamasishe kilimo cha malisho kwa wafugaji, tutumie mashamba darasa kuelimishia wafugaji hakika kilio cha malisho msimu wa kiangazi tutakitokomeza. MAKAMU M/KITI TRSA

Thursday, 2 March 2017

WAFUGAJI WASHIRIKISHWE KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA MIMEA VAMIZI KWENYE NYANDA ZA MALISHO.

Kwa sasa maeneo yetu ya machunga yanazidi kushambuliwa na mimea vamizi. Malisho yanazidi kuteketea kwa sababu ya madhara mbalimbali yanayosababishwa na mimea hii. Hata hivyo, nafikiri elimu ikitolewa kwa mfugaji anayetumia machunga haya tunaweza kupata mafanikio chanya kabisa kuhusu kupunguza kasi ya kutapakaa kwa mimea hii vamizi. Mimea inapovamia eneo husika mfugaji atalazimika kuhama sababu ya malisho kupoteza ubora. Kwanza mfugaji anatakiwa kuelimishwa kuwa mtafiti juu ya mmea wowote ambao hajauzoea ndani ya eneo la ikolojia. Kwa vile hawa wafugaji wanayajua vizuri maeneo yao ya machunga ni rahisi sana kugundua uwepo wa mmea mpya ndani ya eneo, hivo aelimishwe namna ya kuyakabili kwa kuyaondosha kabisa kila yanapojitokeza. Hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia mimea vamizi kusambaa ndani ya machunga kwa sababu itakuwa inaondolewa kila mara inapogunduliwa kujitokeza. MAKAMU M/KITI TRSA

Wednesday, 1 March 2017

HUKU NDIKO TUNAKOTAMANI WAFUGAJI WETU WAFIKE.

Ni ukweli usiopingika kwamba wafugaji wengi wa kitanzania ni wale wenye shughuli hii kama asili yao mfano wasukuma na wamasai. Jamii hizi ndizo zimekuwa chanzo kikubwa cha mifugo na mazao ya mifugo katika masoko na minada yetu hapa nchini na nje ya nchi. Lakini kama ufugaji ndio utamaduni wao je, ni kweli tuna sababu ya kupoteza utamaduni wao? Jibu ni hapana,bali kusaidia kuboresha mfumo wa ufugaji kuhakikisha kuwa mfugaji anafaidika na ufugaji wake wa kila siku kwa ajili ya kuongeza kipato na kustawisha uchumi wa nchi. Mambo makuu mawili kwa mfugaji wa kitanzania yanayomkuba ni mabadiliko ya tabia nchi pamoja na ongezko kubwa la watu ambalo linazidi kuimega ardhi ya malisho kwa shughuli mbalimbali kama makazi na kilimo. Kuendana na hali hii ya mabadiliko kuna kila sababu ya mfugaji kuona sasa umuhimu wa kujikita katika kilimo cha malisho ya mifugo. Hii ina maana kwamba mfugaji atatakiwa kununua ardhi na kujikita katika kilimo cha malisho ili kuhakikisha ustawi wa mifugo yake kwa mwaka mzima. Kilimo hiki kinahitaji ushauri wa kitaalamu haswa kuweza kutambua aina ya majani yanayoweza kustahimili kulingana na eneo analopatikana mfugaji. Ni kweli kuna gharama zake lakini faida yake ni kubwa zaidi kuliko kutangatanga na mifugo katika kipindi ambacho malisho hayapatikanai. .Kilimo cha malisho kinampa mfugaji uwezo wa kuvuna nyasi hadi mara nne kwa mwaka na kujitengenezea uwezo mkubwa wa kuhudumia mifugo yake. Aidha, kilimo cha malisho kitapunguza kutembeza mifugo umbali mrefu zaidi kwa ajili ya kutafuta malisho jambo ambalo huharibu ubora wa nyama, hudhoofisha mifugo na kuipunguzia uwezo wa kuzaliana (reproductive efficiency). Katika msimu wa mvua malisho huwa ni mengi sana, uwezo wa ardhi kuzalisha malisho huongezeka na hivyo mifugo hupata chakula kiurahisi, lakini huu ndio msimu ambao wafugaji wetu wanatakiwa kujifunza namna ya kuhifadhi chakula kwa ajili ya baaadae. Mfano kuacha baadhi ya maeneo bila kuyachunga hadi msimu wa kiangazi ndio yachungiwe ili kuilinda mifugo hadi msimu mwingine.
. Mfugaji anaweza kuvuna pia nyasi na kuziandaa kwa ajili ya hei(HAY) baadae kuzifunga vizuri na kuzitunza hadi msimu wa kiangazi ambapo hakuna malisho kwa wingi. Kama mfugaji atakuwa na uwezo wa kuvuna mara nne kwa mwaka, manake atakuwa na uwezo wa kuzalisha hay nyingi zaidi ili kuilinda mifugo yake msimu wa kiangazi isihangaike na chakula.
. Njia nyingine ni katika mfumo wa saileji(silage), inahitaji utaalamu zaidi lakini mfugaji akiweza kuelekezwa tu basi anaweza kuhifadhi chakula cha mifugo kwa mfumo huu pasipo kupoteza ubora wa chakula hicho. Huku ndiko tunakotamani tuwaone wafugaji wakiamkia huku na kunufaika na ufugaji. Mifugo ni utajiri lakini uelewa huu ni tafsiri iliyo mbali na wafugaji wetu. Dhana ya wingi wa idadi ya mifugo ndiyo dhamira ya wafugaji. Lakini kama wakiruhusu utaalamu uingilie katikati yao watavuna zaidi kwa idadi ndogo tu ya mifugo. Tunayo safari ndefu ya kufika tunakotamani cha msingi ni kutonyosheana mikono na kutafutiana chuki bali kuamka na kumsaidia mfugaji atoke huko aliko na twende naye karne ya 21 tunakokutizama katika mfumo wa kibiashara. Makamu m/kiti TRSA.

MATUMIZI YA MOTO NDANI YA NYANDA ZA MALISHO.

Moto ni silaha mojawapo inayoweza kutumika kwa ajili ya kuboresha hali ya machunga kwa ajili ya mifugo iwapo tu utatumika kiusahihi na kwa kuzingatia taratibu za kutumia moto ndani ya machunga. Ijapokuwa matumizi ya moto ndani ya machunga yana madhara yake lakini zifuatazo ni faida za matumizi ya moto ndani ya machunga. 1.Kutumika kwa ajili ya kuondosha mabaki ya majani yaliyokauka au kujishikiza kwenye vichaka na miti. 2. Kudhibiti mimea vamizi haswa kwa kuua mbegu zinazozalishwa au zilizo kwenye udongo tayari kwa kuota. 3. Kuchochea ukuaji wa malisho haswa msimu wa vuli unapokaribia. 4. Kuvutia mifugo kuweza kula malisho katika sehemu ambazo haipendelei kwenda sababu ya malisho kukosa ubora na virutubisho. 5. Kuua na kudhibiti magonjwa na wadudu wasababishao magonjwa kwa mifugo. 6. Kutumika kuzuia moto usiotarajiwa(wildfire). 7. Kuboresha makazi kwa ajili ya wanyama wafugwao pamoja na wanyama pori n.k Aidha pamoja na hayo, kama ilivyoelezwa mwanzo, matumizi ya moto yana utaratibu wake ndani ya eneo la malisho ya mifugo ama wanyamapori. Lazima mtaalamu wa sayansi ya usimamizi wa nyanda za malisho ajiridhishe kwa kuangalia hali ya hewa, kiasi cha mvuke, aina ya eneo na aiana ya uoto nk. ndio aamue kuhusu kutumia moto kama silaha salama kurekebisha hali ya malisho.